Thursday, December 20, 2012

KIM, RENARD KUONGEA NA VYOMBO VYA HABARI KESHO

Kocha msaidizi wa Zambia (Chipolopolo), Patrice Beaumelle, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana.  Beaumelle amefanana na kocha mkuu Herve Renard kama mapacha.

Makocha Kim Poulsen wa Tanzania (Taifa Stars) na Herve Renard wa Zambia (Chipolopolo) watakuwa na mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Desemba 21 mwaka huu) kuzungumzia pambano lao litakalochezwa Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Makocha hao watazungumzia maandalizi yao ya mwisho kabla ya pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Sylvester Kirwa kuanzia saa 10 kamili jioni.

Pia makocha hao watajibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu pambano hilo litakalokutanisha timu hizo ambazo zimefanya vizuri kwenye orodha ya viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) vilivyotolewa jana (Desemba 19 mwaka huu).

Wakati Zambia ambao ni mabingwa wa Afrika wamepanda juu kwa viwango vya ubora kwa nafasi nne, Taifa Stars ambayo katika mchezo uliopita iliifunga Kenya (Harambee Stars) bao 1-0 imepanda kwa nafasi nne.

Taifa Stars ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini tangu Desemba 12 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo kubwa ya kirafiki inayotarajiwa kuwa ya kuvutia.

No comments:

Post a Comment