Saturday, December 8, 2012

MAGOLI YA KUJIFUNGA YABAKISHA TAJI LA 13 LA CHALENJI UGANDA... TANZANIA BARA YAISHIA YA NNE... BOCCO, NGASSA WENYE MABAO MATANO WANYIMWA TUZO YA UFUNGAJI BORA, APEWA SSENTONGO MWENYE MAGOLI MANNE

Mshambuliaji wa Uganda, Robert Ssentongo (mbele) akimfungisha tela mchezaji wa Kenya wakati wa mechi yao ya fainali ya Kombe la Chalenji kwwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala leo.
Patashika katika mechi ya fainali leo baina ya Uganda na Kenya kwenye Uwanja wa Mandela Kampala. Uganda ilishinda 2-1.

Kocha wa Zanzibar Heroes, Salum Nassoro Bausi, ambaye tayari alishatangaza kujiuzulu baada ya timu hiyo kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali, akibebwa juu na wachezaji wake baada ya kushinda kwa penalti 6-5 dhidi ya Tanzania Bara leo. Dakika 90 za mechi hiyo ziliisha ka sare ya 1-1. 

Wachezaji wa Zanzibar Heroes wakishangilia baada ya kushinda kwa penalti 6-5 dhidi ya Tanzania Bara leo. Dakika 90 za mechi hiyo ziliisha ka sare ya 1-1. 
MAGOLI mawili ya kujifunga kutoka kwa wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, yamewapa wenyeji Uganda (The Cranes) ubingwa wa 13 wa michuano ya mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) kufuatia ushindi wa 2-1 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala leo.

Kwa kutwaa kombe hilo, ambalo ni la nne kwa kocha wao Bobby Williamson, Uganda imeondoka na zawadi ya kwanza ya kombe na dola 30,000 wakati Wakenya walioshina nafasi ya pili wamepata dola 20,000 huku Zanzibar Heroes iliyoshika nafasi ya tatu imepata dola 10,000.

Nyota wa Uganda, Brian Umony ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano hiyo na tuzo ya kipa bora imekwenda kwa kipa wa Uganda, Hamza Muwonge, ambaye ameruhusu goli moja tu katika michuano yote, ambapo Uganda wameshinda mechi zao zote.

Utata umekuja katika tuzo ya mfungaji bora baada ya kupewa Robert Ssentongo wa Uganda, mwenye magoli manne na kuachwa Mrisho Ngassa na John Bocco waliofunga magoli matano kila mmoja.

Rais wa CECAFA, Leodegar Tenga alikuwapo jukwaani kuwakabidhi zawadi washindi.

Zanzibar Heroes ilipata ushindi wa tatu baada ya mapema leo kuwafunga ndugu zao wa Tanzania Bara kwa penalti 6-5, baada ya dakika 90 za mechi yao kumalizika kwa sare ya 1-1.

Tanzania Bara walihitaji kukaza kwa dakika nne tu za mwisho ili kupata ushindi wa 1-0 kupitia goli la mapema dakika ya 10 lililofungwa na Mwinyi Kazimoto kufuatia pasi ya kichwa ya John Bocco.

Lakini mchezaji Abdallah Othman Ali aliyeingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya kiungo Suleyman Kassim 'Selembe', aliisawazishia Zanzibar goli katika dakika ya 86.

Sabri Ali Makame ndiye aliyefunga penalti iliyowapa ushindi Zanzibar baada ya beki Kelvin Yondani kupiga nje penalti yake wakati wa kupigiana penalti moja-moja baada ya tano za kwanza kumalizika huku kila timu ikiwa imefunga nyingine moja-moja ya hatua hiyo ya "piga nikupige".

Katika penalti tano-tano za kwanza kila timu ilikosa penalti moja. Mwinyi Kazimoto alikosa penalti ya nne kwa upande wa Bara iliyodakwa na kipa wa Zanzibar wakati Nasoro Masoud "Chollo" alikosa penalti ya nne ya Zanzibar Heroes iliyodakwa na kipa wa Bara, Juma Kaseja.

Waliopata penalti zao kwa upande wa Bara walikuwa Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shabani Nditi, Shomary Kapombe na Frank Domayo, wakati waliofunga kwa upande wa Zanzibar walikuwa ni Khamis Mcha,  Samih Nuhu, Aggrey Morris, Abdallah Othman Ali, Nadir Haroub 'Cannavaro', na Sabri Ali Makame aliyepiga ya ushindi.      

Timu ya Tanzania Bara inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho Jumapili saa 11:00 kwa ndege ya Precision Air.

No comments:

Post a Comment