Monday, December 10, 2012

KUWA BABA HAKUJAMZUIA MESSI KUENDELEA KUVUNJA REKODI

Messi akishangilia kuvunja rekodi iliyodumu kwa miaka 40 ya Gerd Mueller ya kufunga magoli 86

Messi akishangilia bao la kwanza lililoifikia rekodi ya Gerd Mueller iliyodumu kwa miaka 40.

Messi akishangilia bao lake la kwanza jana ambalo lilikuwa la 85 mwaka 2012

Chezea jini wewe

MADRID, Hispania
MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Lionel Messi alikuwa baba kwa mara ya kwanza mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 25 lakini kuwa mzazi hakukuonyesha kumpunguza kasi Muargentina huyo, zaidi kumuongeza kiu ya mabao.

Mwanasoka Bora wa Dunia Messi alizipita rekodi mbili kwa magoli yake mawili aliyoyafunga katika mechi ya La Liga dhidi ya Real Betis jana, akiipiku ya Gerd Mueller iliyodumu kwa miaka 40 ya kufunga magoli 85 katika mwaka mmoja wa kalenda na pia kuipita rekodi ya Cesar Rodriguez, ambaye aliyecheza katika miaka ya 1940 na '50, na kuwa kinara wa mabao ya ligi katika historia ya Barca akiwa na magoli 192 (ya ligi pekee).

Messi alihitaji mechi 66 kufikisha magoli 86 na kumpiku Mueller, ambaye alifunga magoli yake 85 katika 60 alizoichezea Bayern Munich na timu ya tafa ya Ujerumani mwaka 1972. Messi pia alifikisha jumla ya magoli 192 katika La Liga pekee katika mechi 229 za Barca tangu alipoanza mwaka 2004 na kuwa kinara kwa klabu hiyo, ukilinganisha na anayemfuatia Cesar Rodriguez aliyefunga magoli 190 katika mechi 287 alizoicheza Barca.

Muargentina huyo bado ana mechi mbili za La Liga na moja ya Kombe la Mfalme ya kuzidi kumuacha Ger Mueller kwa mwaka huu 2012 na kama ataendelea kufunga kwa wastani wa mechi zake za sasa, rekodi zake za mabao zitadumu kwa miaka mingi, mingi sana.

"Nitajaribu kufunga goli moja ama mawili zaidi (kabla ya mwisho wa mwaka) ili kuifanya iwe rekodi ngumu zaidi kwa yeyote atakayekuja nyuma yangu kutaka kuivunja," Messi mwenye utani aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi dhidi ya Betis.

Akiitwa kwa jina la utani la "the flea", Messi ameweka utawala ambao unamfunika vibaya mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya nne mfululizo ya Mwanasoka Bora wa Dunia - rekodi nyingine - wakati mshindi atakapotangazwa mwezi ujao.

Mjadala kama yeye ni mwanasoka bora wa wakati wote pengine unaweza kumalizwa kama Messi atapata mafanikio ambayo waliyapata magwiji wa soka Pele na Diego Maradona ya kutwaa Kombe la Dunia.

Swali kwamba Messi hawezi kutisha anapocheza bila ya nyota wenzake wa Barca kama Xavi, Andres Iniesta na Cesc Fabregas limepata majibu kwa kiwango chake cha sasa kwenye timu yake ya taifa ya Argentina.

Magoli yake 12 aliyofunga kwenye mechi tisa zilizopita za timu yake ya taifa mwaka 2012 yameifikia rekodi ya taifa iliyowekwa na Gabriel Batistuta na anayo fursa ya kuhitimisha kwamba yeye ni gwiji wa soka wakati Brazil itakapoandaa fainali za Kombe la Dunia 2014.

Umuhimu wa Messi kwenye nafasi ya Barca kutwaa taji lolote msimu huu hauna maswali.

Magoli yake mawili aliyofunga jana yalimfanya afikishe jumla ya magoli 23 katika mechi 15 za La Liga msimu huu, ambayo ni takribani nusu ya jumla ya magoli 50 aliyomfunga msimu mzima uliopita, na amewasaidia kushinda mechi zote isipokuwa moja dhidi ya Real Madrid na kuwa pointi 43, sita juu ya Atletico Madrid walio katika nafasi ya pili katika msimamo.

Alifunga magoli 50 kati ya mabao 114 ya Barca katika La Liga msimu uliopita - ambayo yaliweka rekodi ya mabao Hispania - na alifunga mabao 31 katika ya 95 msimu wa 2010-11 na amekuwa mfungaji bora wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa misimu minne mfululizo iliyopita, wakati Barca imetwaa ubingwa huo wa Ulaya mara mbili.

"Hakika, tutathmini rekodi la Leo kwa kadri miaka inavyokwenda," mkurugenzi wa michezo wa Barca, Andoni Zubizarreta, ambaye bila ya shaka anashukuru kwamba Messi hakuwapo enzi zake wakati akiwa mlinda mlango wa Barca na timu ya taifa ya Hispania, alisema katika mahojiano na TV Jumapili.

"Daima atasema kwamba magoli yake ni matokeo ya kazi ya pamoja na wenzake, kwamba ni juhudi za timu nzima, lakini kipaji cha kufunga ni chake peke yake," aliongeza.

"Kwa yeyote anayependa soka, kumuangalia Leo uwanjani ni bahati kubwa."

No comments:

Post a Comment