Wednesday, December 19, 2012

KOCHA VILANOVA WA BARCELONA AREJEWA NA SARATANI... WACHEZAJI HOFU ZAPANDA

Tivo Vilanova

Tivo Vilanova

Tivo Vilanova

Tivo Vilanova akiwa mzigoni

Tivo Vilanova (kulia) akisalimiana na kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho

MADRID, Hispania
KOCHA wa Barcelona, Tito Vilanova amerejewa na ugonjwa wa saratani katika vifuko vya kuhifadhia mate, gazeti la kila siku la Hispania la El Pais limeripoti leo likiegemea katika vyanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.

Vilanova (44), ambaye alifanyiwa upasuaji wa vifuko hivyo Novemba mwaka jana, alipanda ngazi kutoka katika nafasi yake ya ukocha msaidizi na kuchukua nafasi ya Pep Guardiola kama kocha mkuu msimu huu.

Vinara hao wa La Liga walitoa taarifa ya kufuta hafla yao ya Krismasi iliyopangwa kufanyika pamoja na vyombo vya habari na rais Sandro Rosell asubuhi ya leo, wakisema sababu zitatajwa baadaye.

"Najisikia vibaya sana kwa taarifa hizi," kiungo wa Barca, Xavi alisema katika ukurasa wake rasmi wa Twitter, huku meseji za pole zikimiminika.

Mcheza tenisi namba moja duniani wa zamani Rafa Nadal alisema: "Nguvu yangu yote na sapoti kwa Tito Vilanova! Sote tuko pamoja nawe kukiruka kikwazo hiki kingine."

Vilanova alikuwa nje ya kazi yake kwa wiki tatu baada ya kufanyiwa upasuaji huo mwaka jana, lakini alirejea 'mzigoni' kumsaidia Guardiola katika miezi yake sita ya mwisho ya msimu wa 2011-12.

Mcatalunya huyo anayezungumza kwa upole alisema upasuaji huo ulimpa uzoefu tofauti katika suala la maisha, wakati akitambulishwa mwezi Juni.

"Nilifanyiwa upasuaji muhimu sana miezi michache iliyopita," alisema. "Nilizungumza na madaktari na familia yangu kuhusu ajira hii, lakini wote waliniambia kwamba niko fiti kabisa na kwamba hakuna tatizo.

"Kupona kutoka katika upasuaji ule kulinipa mtazamo tofauti kuhusu maisha. Hata hivyo, baada ya yote yaliyotokea, kufanya mazoezi na Barca kutakuwa kama watoto walio mchezoni."

Vilanova ameiwezesha timu yake kuongoza La Liga kwa kushinda mechi 15 kati ya 16, pointi tisa juu ya Atletico Madrid wanaoshika nafasi ya pili, na kutinga katika hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kama vinara.

Barca imebakisha mechi moja, ugenini dhidi ya Valladolid katika La Liga Jumamosi, kabla ya mapumziko ya wiki mbili ya kupisha majira ya baridi.

No comments:

Post a Comment