Wednesday, December 19, 2012

ZAMBIA WATUA DAR NA “MUZIKI MUNENE’ KUIVAA TAIFA STARS JUMAMOSI … WANAONGOZWA NA NAHODHA WAO CHRIS KATONGO ALIYEWABWAGA DIDIER DROGBA NA YAYA TOURE KABLA YA KUTWAA TUZO YA BBC YA MWANASOKA BORA WA AFRIKA 2012…!

Katongo na wenzake wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa jijini Dar es Salaam leo Desemba 19, 2012.
Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo), Patrice Beaumelle akizungumza na waandishi baada ya kutua Dar. Beaumelle amefanana sana na kocha mkuu wa timu hiyo Herve Renard.
Baadhi ya wachezaji wa Zambia wakiwa kwenye uwanja wa ndege jijini Da leo Desemba 19, 2012.
Ndani ya Dar... Christopher Katongo akibusu mfano wa Tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika wakati akiwa mazoezini na wenzake jijini Lusaka, Zambia jana. Mkali huyo na wenzake wameshatua jijini Dar kujiandaa na mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Taifa Stars.
Wachezaji wa kikosi cha Zambia wakitafakari wakati wakiwa mazoezini jijini Lusaka jana kabla ya kutua jijini Dar es Salaam leo (Desemba 19, 2012) ili kuivaa Taifa Stars katika mechi yao ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi.
Katongo na wenzake
Katongo akizungumza na wanahabari baada ya kuwasili

Katongo akizungumza na wanahabari baada ya kuwasili

Wachezaji wa Chipolopolo wakiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere leo jioni

Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Zambia, Patrice Beaumelle akizungumza na waandishi baada ya kutua Dar. Beaumelle amefanana sana na kocha mkuu wa timu hiyo Herve Renard.


Nahodha Christopher Katongo ambaye juzi aliwashinda Didier Drogba wa Shanghai Shenhua na Yaya Toure wa Manchester City na kutwaa Tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika ni miongoni mwa nyota wa mabingwa wa Afrika, Zambia “Chipolopolo” waliotua jijini Dar es Salaam jioni hii kwa ajili ya kucheza mechi yao ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa “Taifa Stars” itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Katongo na wenzake wametua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mishale ya saa 11:45, wakiwa pia na kocha  Mfaransa Herve Renard, ambaye ndiye aliyewasaidia kuishangaza dunia kwa kutwaa ubingwa wa Afrika 2012 katika fainali waliyoshinda kwa penati dhidi ya Ivory Coast nchini Gabon.
Mbali na Katongo, nyota wengine waliotua leo ni pamoja nyota wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rainford Kalaba na Given Singuluma ambaye ni  mfungaji bora wa fainali za kwanza za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).

Wengine ni Chintu Kampamba, Chisamba Lungu, Danny Munyau, Davy Kaumbwa, Derrick Mwansa, Evans Kangwa, Felix Katongo na Francis Kasonde, Hichani Himonde, Isaac Chansa, James Chamanga, Jimmy Chisenga, Jonas Sakuwaha, Joshua Titima, Kalililo Kakonje, Moses Phiri, Mukuka Mulenga, Rainford Kalaba, Roderick Kabwe na  Salulani Phiri.

Hata hivyo, beki Stopilla Sunzu wa klabu ya TP Mazembe ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mwaka 2012, si miongoni mwa wachezaji waliotua nchini jioni hii, leo Desemba 19, 2012 na kocha Renard amesema atakuja kivyake kwani ameenda Accra, Ghana kushiriki katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Mwanasoka Bora wa Afrika zinazoandaliwa na Shirikishon la Soka (CAF).

Sunzu anawania Tuzo ya Mwansoka Bora miongoni mwa nyota wa Afrika wanaocheza ligi za ndani.


Akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Katongo alisema kuwa Stars imezidi kuimarika katika siku za hivi karibuni na kucheza soka safi; hivyo hawatarajii kupata mteremko.


“Tunashukuru sana kupata mwaliko wa kuja kucheza Tanzania… nadhani itakuwa mechi yenye ushindani mkali. Tumejiandaa vizuri maana tumeiona timu ya Tanzania ikicheza soka safi na kuzipa shida timu kubwa barani Afrika,” alisema Katongo.


“ Sisi ni mabingwa wa Afrika na hivyo wengi wanatuangalia kuona tutafanya nini mwaka huu baada ya mwaka uliopita kufanya vizuri sana.


“Tunahitaji kujiandaa vizuri zaidi ili kutetea ubingwa wetu na mechi hii (dhidi ya Stars) ni sehemu mojawapo ya maandalizi yetu,” alisema Katongo, mshindi wa Tuzo ya BBC ya Mwansoka Bora wa Afrika 2012.


Kocha aliyeisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa fainali zilizopita za Afrika (Afcon 2012) zilizofanyika Equatorial Guinea na Gabon mwanzoni mwa mwaka huu, Herve Renard, alisema vilevile kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kwao kwa sababu Tanzania inakuja juu kisoka.


“Tanzania kwa sasa inacheza soka safi na si timu ya kubeza hata kidogo. Tunafurahi kupata mwaliko wa kuja kucheza nao,” alisema.

“Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi yetu kuelekea kwenye michuano mikubwa inayotukabili (fainali za Afcon 2013)… tutaonyesha soka zuri, alisema.

“Kikosi tulichokuja nacho kina asilimia 60 ya wachezaji ambao walishiriki katika kutwaa ubingwa wa Afrika. Naamini tutafanya vizuri,” aliongeza Renard mwenye umri wa miaka 43.Akieleza zaidi, kocha huyo alisema kuwa nyota wake mwingine, beki Stopilla  Sunzu wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo atakuja peke yake baadaye kwa sababu ameenda nchini Ghana kuhudhuria utoaji wa Tuzo za Wanasoka Bora wa Afrika Mwaka 2012 zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

KIINGILIO
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa kiingilio cha chini katika mechi hiyo ya Jumamosi itakayoanza saa 10:00 jioni kitakuwa Sh. 5,000 wakati cha juu kitakuwa Sh. 30,000.

No comments:

Post a Comment