Wednesday, December 19, 2012

KINA CANNAVARO RUKSA KUWAVAA KINA KATONGO

Wachezaji wa Zanzibar Heroes wakishangilia baada ya kuifunga Tanzania Bara kwa penalti 6-5 katika mechi yao ya kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Mandela mjini Kampala, Uganda.

WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Zanzibar waliofungiwa mwaka mmoja na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kucheza soka mahala popote kutokana na madai ya utovu wa nidhamu, wako huru kuendelea kuzitumikia klabu zao hadi Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakapokaa kujadili adhabu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF leo, shirikisho hilo limepokea barua ya ZFA inayowafahamisha kuhusu adhabu zilizotolewa kwa wachezaji hao.

Hata hivyo, TFF imesema imelipeleka suala hilo katika Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF kwa hatua zaidi, "hivyo kwa sasa shirikisho litasubiri uamuzi wa kamati hiyo".  

Hatua hiyo inamaanisha kwamba nyota wa Zanzibar walio katika kambi ya timu ya taifa (Taifa Stars) wataendelea kuitumikia timu hiyo katika kujiandaa kuwakabili mabingwa wa Afrika, Zambia 'Chipolopolo' katika mechi ya kirafiki itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Baadhi ya wachezaji waliofungiwa ni nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Aggrey Morris, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nassoro Masoud Cholo, Mcha Khamis, Mwadini Ali, Seif Abdallah na Selemani Kassim 'Selembe'.

Kamati ya Utendaji ya ZFA iliwafungia wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwa kitendo chao cha kuamua kugawana zawadi ya Dola 10,000 walizopata baada ya kushinda nafasi ya tatu ya mashindano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) 2012 baada ya kuwafunga ndugu zao wa Tanzania Bara kwa penalti 6-5 mwezi uliopita nchini Uganda.

Licha ya ZFA kutangaza adhabu hiyo, wachezaji wote wameendelea kujifua katika klabu zao na hata timu ya taifa (Taifa Stars), jambo lililoonyesha kukichefua chama hicho cha soka cha Zanzibar, ambacho kimelalamikia kupuuzwa na TFF. 

Hata hivyo, maamuzi ya kuwafungia wachezaji hao kuchezea hadi klabu zao yamewashangaza wengi yakionekana kuwa ni ya jazba zaidi kwani chama cha soka hakiwezi kumzuia mchezaji kuitumikia klabu yake iliyomuajiri.  
No comments:

Post a Comment