Thursday, December 20, 2012

HOTELI LA DOUBLE TREE HILTON JIJINI DAR ES SALAAM YAFUNGWA KWA KUTIRIRISHA KINYESI BAHARINI... NI HOTELI KALI LA HADHI YA NYOTA TANO LILILOPO UFUKWENI MWA BAHARI OYSTERBAY.. NI BAADA YA KUKAIDI AGIZO LA SIKU SABA KUKOMESHA UCHAFUZI HUO WA MAZINGIRA

Hoteli ya Doule Tree Hilton inavyoonekana kwa mbele. Eti 'mizigo' yote ya wateja wa hoteli hii kali iliyopo Oysterbay imekuwa ikitiririshwa baharini!
Khaaa...! Nyie vipi? Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Dk. Terezya Huvisa (katikati) akitoa maelekezo kwa viongozi wa hoteli ya Double Tree baada ya kuifunga rasmi jana kutokana na kosa la kutiririsha vinyesi vya wateja wake baharini. 
Onavyoonekana kwa karibu.
Muonekano wake kwa nyuma
Eneo lake la bwawa la kuogelea.
Moja kati ya vyumba vya hoteli ya Double Tree iliyoko Oysterbay ambayo imefungiwa kuanzia jana (Desemba 19, 2012) baada ya kubainika kuwa vinyesi katika hoteli hiyo vimekuwa vikitiririshwa baharini.Waziri Dk. Huvisa akikagua baadhi ya miundombinu ya hoteli ya Double Tree jana kabla ya kutangaza kuifunga hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tano.


Serikali imeifungia hoteli ya kitalii ya Double Tree by Hilton ya jijini Dar es Salaam kutokana na kukaidi agizo la kuacha kutiririsha majitaka baharini.

Hatua hiyo ilichukuliwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa.

Hoteli hiyo ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano iko Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Huvisa alitoa agizo la kuifunga hoteli hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga.

Ziara hiyo ililenga kuona utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa awali na Kitwanga Desemba 6, mwaka huu, alipofanya ziara kutembelea viwanda na hoteli zilizoko pembezoni mwa bahari ya Hindi kuona mfumo wa majitaka.

Katika ziara hiyo, Kitwanga aliiagiza hoteli hiyo kuwa na mpango wa muda mfupi na wa haraka wa kusitisha utiririshaji wa maji taka baharini, lakini hadi kufikia jana agizo hilo halikutekelezwa.

Mbali na kuifunga, Waziri Huvisa pia alifuta hati ya ukaguzi wa Mazingira (Environemental Audit) na kuitaka hoteli hiyo kurekebisha mara moja mfumo huo na pia kulipa faini kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).

Waziri Huvisa alisema hoteli hiyo itafunguliwa baada ya kutekeleza maagizo ya serikali.

Wakati wa ziara ya Naibu Waziri Kitwanga katika hoteli hiyo, ilibainika kwamba mfumo wa majitaka haujajengwa vizuri kuruhusu maji hayo kusafishwa kabla hayajamwagwa au kuingizwa kwenye mfumo wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco).

Kitwanga na maofisa wa Nemc walifika kwenye hoteli na kuhoji mfumo wa majitaka pamoja na sababu za kujengwa hadi baharini.

Mameneja wa hoteli hiyo walimweleza Naibu Waziri kwamba maji hayo yanahifadhiwa vyema kisha kuzolewa kwa magari ambayo huenda kuyamwaga kwenye mabwawa ya majitaka.

Hata hivyo, Kitwanga alihoji linapopita gari la kwenda kuchukua maji hayo kwa kuwa eneo zima limezungukwa na majengo pamoja na ukuta usioruhusu gari kupita.

Baada ya kuendelea kukagua, ndipo ilibainika kwamba uchafu wote wa hoteli hiyo na hasa maji ya chooni yanamwagwa baharini.

“Tulichoona hapa ni kinyesi kabisa, harufu ya maji ya chooni inatoka halafu hawa wanatudanganya eti ni mtiririko wa maji wa kawaida, hali hii haikubaliki," alisema Kitwanga alipofanya ziara hiyo.

Kitwanga alisema serikali inawahamasisha wawekezaji waje kuwekeza nchini, lakini kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu na kwamba, vinginevyo itawachukulia hatua stahiki.

Alimweleza Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Sven Lippinghof,  kumwaga kinyesi baharini ni suala lisilovumilika na kumtaka kuzingatia sheria ya mazingira na nyinginezo ili kulinda afya ya viumbe wa baharini na za wananchi.

Naibu Waziri huyo aliitaka Nemc kufuatilia kwa kina usitishwaji wa kumwaga maji hayo na kumpa mwekezaji huyo wiki moja kwamba hadi Desemba 14, mwaka huu awe amefanya marekebisho ya kina.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Nemc, Manchere Heche, aliitaka hoteli hiyo kusitisha kumwaga maji hayo baharini kuanzia siku hiyo na kumwandikia barua ya kusisitiza amri hiyo.

Alisema kuanzia Desemba 6 Nemc ingefanya ukaguzi katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba agizo hilo linatekelezwa.

Alisema: “Afya za watu haziwezi kusubiri muda, na tutawatoza faini kwa uchafuzi huu wa mazingira.”

Kwa upande wake, Lippinghof alisema atatekeleza maagizo hayo ya Nemc na kwamba suala la kuzingatia sheria halina mjadala.

Alisema atawasilisha pia maagizo hayo kwenye kikao cha bodi ya wakurugenzi wa hoteli hiyo kwa hatua zaidi.

No comments:

Post a Comment