Wachezaji wa Kilimanjaro Stars wakirejea kwenye Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo |
TIMU ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) iliyoshiriki katika michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) iliyomalizika mjini Kampala juzi Jumamosi, imerejea Jijini Dar es Salaam leo.
Stars, ambayo inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, imerejea leo jioni kwa ndege ya Precision Air ikiwa na wachezaji 18 walioiwezesha kushika nafasi ya nne baada ya kufungwa na ndugu zao wa Zanzibar Heroes kwa penalti 6-5 katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu.
Wenyeji Uganda (The Cranes) walitetea taji lao na kulibakisha kombe hilo kwa mara ya 13.
Akizungumza baada ya kurejea, kocha wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen alisema mashindano haya yalikuwa muhimu sana kwa timu yake kwani vijana wamepata uzoefu baada ya kukutana na timu ngumu na zenye uzoefu.
“Mashindano yalikuwa mazuri…tulienda na nia ya kurudi na kombe lakini hatujafanya hivyo ila muhimu ni kwamba mashindano haya yametupa uzoefu mkubwa ili tuweze kujiandaa na mashindano mengine ambayo yako mbele yetu,” alisema.
“Tumefarajika kucheza dhidi ya timu kubwa kama The Cranes ambayo ndio timu bora katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati,” alisema.
Aliongeza kuwa hivi sasa macho ya wachezaji yote yako katika mechi yao ya ijayo ya kirafiki dhidi ya Chipolopolo ya Zambia.
"Nawaomba Watanzania wasikate tama kwa kuwa tunaijenga timu. Hawa ni vijana na ninaamini siku zijazo watafanya vizuri zaidi,” alisema Poulsen.
Kocha huyo anatarajiwa kutangaza kikosi cha Taifa Stars kesho na amesema atawaita wachezaji wa Zanzibar pia ambao walicheza vizuri Kampala.
“Niliwaona wakicheza kwa hivyo bila shaka waliofanya vizuri watakuwamo kwenye kikosi hiki,” alisema Mdenmark huyo.
No comments:
Post a Comment