Monday, December 31, 2012

KOCHA MFARANSA ATUA SIMBA NA KUAHIDI MAKUBWA

Kocha wa Simba, Mfaransa Liewig akizungumza na waandishi baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Desemba 31, 2012.
Kocha mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig ametua nchini leo na kupokewa na mamia ya mashabiki wa 'Wanamsimbazi' huku akiahidi kuwaletea mafanikio makubwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Liewig aliyekuja kutwaa nafasi iliyoachwa wazi na Mserbia Milovan Cirkovic, amesema 'Wanamsimbazi' watarajie mambo mazuri kutoka kwake, lakini kwa sharti la kumpa ushirikiano katika kila hatua wakati atakaposaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo na kuanza kibarua chake.

"Nimefurahishwa sana na mapokezi haya... najihisi kuwa nina deni kubwa. Naamini nitapata ushirikiano wa kutosha na baada ya kuzoeana na wachezaji, naamini Simba itafika mbali katika kila michuano," alisema kocha huyo.

Miongoni mwa watu waliofika uwanjani kumpokea kocha huyo ni Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, ambaye aliwaongoza mamia ya mashabiki wa Simba kumpokea kwa maandamano ya magari na pikipiki za bodaboda na bajaji.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa kocha huyo atasaini mkataba wa kuifundisha klabu hiyo kwa miezi 18 na tukio hilo litakamilishwa kesho.

No comments:

Post a Comment