Tuesday, December 25, 2012

KRISMASI NJEMA MASTRAIKA.... NA SOKA KESHO LINAENDELEA

Happy Krismasi mastraikaaaaaaa..............

VINARA wa Ligi Kuu ya England, Manchester United watawania kuongeza tofauti yao ya pointi nne kileleni wakati watakapowakaribisha Newcastle katika 'Boxing Day' iliyojaa mechi za ligi hiyo kesho.

Mabingwa Manchester City watajaribu kuendelea kupambana wakati watakapocheza dhidi ya Sunderland.

Mkiani mwa ligi, Reading wanaoshika mkia watatarajia ushindi wanaouhitaji sana nyumbani dhidi ya Swansea wakati QPR watawakabili West Brom.

Baada ya wikiendi iliyoshuhudia klabu za mji wa Manchester zikihaha katika mechi zao ambapo Man City walihitaji goli la dakika ya 92 kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Reading huku Man Utd wakishikiliwa kwa sare ya 1-1 na Swansea, Boxing Day inaweza kushuhudia mabadiliko zaidi katika mbio za ubingwa huku timu hizo zikitofautiana kwa pointi nne.

Klabu zote zilishindwa kupata ushindi katika mechi zao za Boxing Day mwaka jana, na makocha Sir Alex Ferguson na Roberto Mancini watahitaji kuona jambo hilo halijirudii kesho.

Akitokea kuisambaratisha Aston Villa kwa magoli 8-0, kocha Rafael Benitez ataipeleka timu yake inayoshika nafasi ya tatu ya Chelsea ugenini Norwich akifahamu kwamba ana rekodi nzuri ya ushindi kwenye mechi za Boxing Day akiwa kama kocha wa ligi kuu ya England kutokana na kushinda mechi tano kati ya sita.

Hakuna timu ambayo imetoka sare nyingi katika kipindi cha sikukuu hizi zaidi ya klabu ya zamani ya Benitez ya Liverpool, na kocha wao wa sasa Brendan Rodgers atajaribu kufukia rekodi hiyo katika mechi yao ya ugenini kesho dhidi ya Stoke.

Fulham pia watajaribu kuzinduka kutoka katika mwendo mbaya ambao ni pamoja na kushinda mechi moja tu kati ya 10 zilizopita wakati watakapowakaribisha Southampton Craven Cottage.

Wakati mechi ya Arsenal dhidi ya West Ham ikiwa imeahirishwa kutokana na uwezekano wa madereva wa treni za ardhini za London kugoma, mahasimu wao katika mbio za kuwania kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, Everton na Tottenham watajaribu kuongeza pointi kwa kucheza dhidi ya Wigan na Villa.


No comments:

Post a Comment