Sunday, November 11, 2012

YANGA YAZIDI KUWAACHIA MANYOYA... YAWAPIGA COASTAL UNION 2-0, CHEZEA DIDIER KAVUMBAGU WEWE?

Hamisi Kiiza 'Diego' wa Yanga akimiliki mpira huku akifuatwa na Juma Jabu wa Coastal Union wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo

YANGA imehitimisha duru la kwanza la Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa kileleni kwa faida ya pointi tano zaidi baada ya kuifunga Coastal Union mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kufikisha pointi 29. 

"Shujaa asiyetajwa sana midomoni" mwa mashabiki wa Yanga, Didier Kavumbagu alifunga goli lake la nane katika ligi msimu huu na kurejea kuongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara sawa na Kipre Tchetche wa Azam, kabla ya Mganda Hamis Kiiza kuongeza la pili wakati Yanga ilipowanyanyasa Coastal kwenye ngome yao.
  
Ushindi wa kujiamini wa leo, umemaanisha kwanza Yanga iliyoanza msimu vibaya kwa vipigo viwili na sare moja katika mechi zake nne za kwanza, inaenda mapumziko "marefu mno" ya mwisho wa mzunguko wa kwanza wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano juu ya Azam wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 24, ambao jana walikalishwa kwenye uwanja huo mgumu kwa kipigo cha 2-1 dhidi ya Mgambo JKT.


Mahasimu Simba, ambao wamedondosha pointi 4 kwenye uwanja huo msimu huu baada ya kushikiliwa kwa sare dhidi ya Coastal na Mgambo, wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 23 na wanafuatiwa kwa karibu na Coastal wenye pointi 22.

Yanga walitumia vyema udhaifu wa migogoro inayoendelea kwa wapinzani wao, Simba na Azam, kwa kucheza soka la kujiamini na kupata ushindi huo uliomkosha kocha wao Mholanzi Ernie Brandts, aliyeajiriwa kuchukua mikoba ya Mbelgiji Tom Saintfiet aliyetimuliwa baada ya mwanzo mbaya wa msimu uliowashuhudia wakizagaa mkiani mwa msimamo.

"Nimefurahi tumeshinda hapa kwa sababu Mkwakwani ni mahala pagumu na timu hudondosha pointi," alisema Brandts akiwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kutawala mechi kwa muda mwingi.

Mholanzi huyo alisema hata hivyo watakitumia kipindi cha mapumziko ya mzunguko wa kwanza kujifua zaidi ili wakirejea waendelee kushinda na pia wacheze soka linalovutia.

Kocha wa Coastal, Hemed Morocco, alisema Yanga walistahili kushinda kutokana na soka walilocheza na kwamba timu yake iliangushwa na kukosekana kwa nyota wao majeruhi Nsa Job na Pius Kisambale, lakini watajiimarisha kwa kuongeza nguvu katika kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Katika uwanja uliofurika mashabiki licha ya kiingilio cha juu kuwa Sh. 15,000 ambacho ni rekodi kulinganisha na kiingilio cha Sh.10,000 wakati Coastal walipocheza dhidi ya Simba, Yanga ilipata goli la kwanza katika dakika 29 kupitia kwa Kavumbagu aliyeitumia vyema pasi ya kiungo Haruna Niyonzima, awali mfungaji akipiga shuti la karibu lililookolewa kabla ya kuuwahi mpira uliorudi na kuutumbukiza kwenye nyavu ndogo kwa chini.  

Mpira wa kurusha kama kona kutoka kwa beki Mbuyu Twite, ulitumbukizwa wavuni na Kiiza kwa kichwa cha kudokoa baada ya kumparaza kichwani Kavumbagu na kuipa Yanga goli la pili katika dakika ya 61.

Coastal ilikaribia kupata goli katika dakika ya 86 wakati kiungo wa zamani wa Simba, Jerry Santo alipopiga kichwa kikali cha jirani na lango lakini kipa Ali Mustapha 'Barthez' aliokoa kishujaa na kuamsha shangwe kubwa kwenye uwanjani humo. 

Yanga pia walikuwa na nafasi nyingi za kufunga zikiwa katika dakika ya 44 wakati Kiiza alipopiga nje kichwa kufuatia krosi safi kutoka kwa Oscar Joshua, kipa wa Juma Mpongo alidaka kiufundi mpira miguuni mwa Kavumbagu aliyekuwa akijiandaa kufunga katika dakika 45 na Mpongo tena akaficha vyema shuti la kustukiza la Kiiza katika dakika 68.

Wageni walitawala tangu mapema nakupata kona katika dakika za 3, 4, 5 na 15 kabla ya shuti la Mkenya Santo kuzaa kona ya kwanza wa Coastal katika dakika ya 20.

'Tiktaka' safi ya Cannavaro ilidakwa na Mpongo katika dakika ya 15 kufuatia kona ya Twite na dakika mbili baadaye Mpongo alidaka 'tiktaka' nyingine ya Frank Domayo iliyotokana na krosi ya Niyonzima, huku kipa wa Yanga, Barthez, akionekana hana kazi ya kufanya kwa muda mwingi wa mwanzo wa mchezo. 

Mechi pekee zilizobaki kwa mzunguko huu ni za Prison ya Mbeya ambayo wachezaji wake walipata ajali. Hawajacheza dhidi ya Ruvu Shootings na Mgambo JKT ya Tanga.

Baada ya mechi hizo, ligi itasimama hadi Januari 26, 2012.

Vikosi vilikuwa: 
Coastal: 
Juma Mpongo, Ismail Khamis, Jamal Machelanga/ Athuman Tamim (dk. 45), Jerry Santo, Mohammed Athuman, Razack Khalfan, Daniel Lyanga, Green Atupele/ Lameck Mbonde (dk. 68) na Seleman Kassim 'Selembe'

Yanga: 
Ali Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Nurdin Bakari, Oscar Joshua, Frank Domayo, Didier Kavumbagu/ Said Banahunzi (dk. 81), Hamis Kiiza na David Luhende.

No comments:

Post a Comment