Monday, November 12, 2012

MESSI AVUNJA REKODI YA PELE... BADO MAGOLI 9 KUWEKA REKODI YA DUNIA

Lionel Messi wa FC Barcelona akishangilia baada ya kufunga goli la nne la timu yake lililovunja rekodi ya Pele wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Real Mallorca kwenye Uwanja wa Iberostar mjini Mallorca, Hispania jana usiku Novemba 11, 2012. Barca ilishinda 4-2.

NYOTA wa Barcelona, Lionel Messi, amevunja rekodi iliyowekwa na gwiji wa Brazil, Pele, baada ya kufunga magoli mawili yaliyoisaidia timu yake kushinda 4-2 ugenini usiku wa kuamkia leo dhidi ya Real Mallorca.

Messi sasa amefikisha magoli 76 katika mwaka 2012, moja zaidi ya rekodi iliyowekwa na Pele mwaka 1958. 


Pele aliweka rekodi hiyo katika mechi 53 alizoichezea klabu yake ya Santos na timu ya taifa ya Brazil, wakati Messi ametumia mechi 59 alizoichezea klabu yake ya Barcelona na timu yake ya taifa ya Argentina.

“Leo anaendelea kuvunja rekodi. Jumla ya mabao yake ni babkubwa. Inawahitaji wachezaji wengine wakubwa misimu saba hadi nane kufunga idadi ya magoli anayofunga katika msimu mmoja. Pia, baadhi ya magoli yake ni makali sana,” alisifu kocha wa Barcelona Toto Vilanova.

Messi sasa amebakisha magoli 9 kufikia rekodi ya wakati wote iliyowekwa na gwiji wa Ujerumani, Gerd Muller, ambaye alifunga magoli 85 katika msimu wa mwaka 1972. Hata hivyo, rekodi ya Muller haipewi nafasi sana kwa sababu magoli 12 kati ya hayo 85, aliyafunga katika michuano ya Football League Cup, ambayo haikuwa michuano rasmi wakati huo.

Barca pia imefikia rekodi ya La Liga ya kuwa na mwanzo mzuri zaidi wa msimu kutokana na kushinda mechi 10 na sare moja, rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Real Madrid katika misimu miwili ya 1968-69 na 1991-92.

No comments:

Post a Comment