Friday, November 9, 2012

TFF YAPONGEZA UONGOZI MPYA FA MWANZA


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeupongeza uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 8 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa leo na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura imesema ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa MZFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika Mkoa wa Mwanza.

"TFF inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati za Utendaji ya MZFA iliyochaguliwa chini ya uenyekiti wa Patrick Songora aliyechaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo," ilisema taarifa hiyo.

Aidha TFF ilisema uongozi huo mpya wa MZFA una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya chama chao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.

"Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF," iliongeza taarifa hiyo.

Viongozi waliochaguliwa kuongoza MZFA ni Patrick Songora (Mwenyekiti), Nassoro Mabrouk (Katibu) na Richard Kadutu (Mwakilishi wa Klabu TFF).
 

No comments:

Post a Comment