Friday, November 9, 2012

MALAWI WAALIKWA PEKEE CHALENJI.... CAMEROON, ZIMBABWE ZATOSWA


MALAWI watakuwa timu pekee waalikwa katika michuano ya Chalenji itakayochezwa Kampala Uganda kuanzia Novemba 24.

Nchi tatu zikiwamo Cameroon na Zimbabwe zilionyesha nia ya kushiriki katika michuano hiyo lakini kamati ya maandalizi imevutiwa na Malawi.

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye amethibitisha jambo hilo akisema Malawi daima imeonyesha ushirikiano mzuri, nidhami na ushindani katika michuano hiyo. Hii itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kwa Malawi kushiriki kama timu mwalikwa tangu mwaka 2010.

Malawi inachukua nafasi ya Djibouti, nchi mwanachama ambayo ilijitoa kwenye michuano kutokana na matatizo ya kiutawala nyumbani. Djibouti inatarajia kufanya uchaguzi wa kumpata rais mpya wa chama cha soka cha nchi hiyo kesho chini ya usimamizi wa maafisa wa FIFA. Memba wa Kamati ya Waamuzi ya Cecafa Houssein Waberi amekuwa mgombea pekee wa kiti hicho.

Makundi ya michuano ya hiyo inayodhaminiwa na bia ya Tusker yatapangwa mjini Kampala Jumatatu. Nchi nyingine shiriki ni Tanzania, Sudan Kusini, Ethiopia, Rwanda, Sudan, Burundi, Eritrea, Somalia, Zanzibar, Kenya na wenyeji Uganda.

Timu ya taifa ya Somalia imewasili mjini Kampala leo kwa ajili ya kuweka kambi nchini humo kujiandaa na michuano hiyo. Ujumbe wa awali kutoka Mogadishu tayari umetua mjini Kampala kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu. 

No comments:

Post a Comment