Saturday, November 10, 2012

SIMBA AFA TENA, TOTO LA YANGA LAIBUKA KIDEDEA.... KOCHA MILOVAN ASEMA KIPA MWETA KAWAFUNGISHA

Mashabiki wa Simba walipoandamana wiki hii baada ya timu yao kufungwa mechi ya kwanza msimu huu dhidi ya Mtibwa

Ndivyo ilivyokuwa kwenye uwasnja wa Mkwakwani Tanga wakati Azam wakipigwa 2-1 leo Novemba 10, 2012.

Okwi wa Simba akidhibitiwa na beki wa Toto (kulia) huku Mwinyi Kazimoto (kushoto) akishuhudia kwa mbali wakati wa mecjhi yao ya ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo novemba 10, 2012.

Simama huko....! Emmanuel Okwi wa Simba (kushoto) akidhibitiwa na beki ngangari wa Toto African wakati wa mechi yao ya Ligi Kuui ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Sekeseke wakati Azam wakifa mbele ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga leo.
Abdulhalim Humud wa Azam (kushoto) akiwatoka wachezaji wa Mgambo JKT wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, leo Novemba 10, 2012. Azam ilichapwa 2-1.
MOTO wa matatizo katika klabu ya Simba umemwagiwa petroli leo kufuatia kipigo cha pili mfululizo kutoka kwa timu inayochechemea ya Toto African kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mashabiki wa Simba waliandamana kwenye makao makuu ya klabu hiyo mwanzoni mwa wiki hii kufuatia timu yao kukumbana na kipigo cha kwanza msimu huu cha 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro na matokeo ya leo yanatarajiwa kuitingisha zaidi timu hiyo.

Wakiwa na jazba, mashabiki mwanzoni mwa wiki walibeba mabango yakiwamo yanayoshinikiza kipa mzoefu, Juma Kaseja na Katibu Mkuu Goffrey Kaburu 'Nyange' waondoke "wawachie Simba yao", lakini mambo si mambo leo baada ya kocha Mserbia Milovan Cirkovic kumbwagia lawama kipa aliyecheza leo kwa mara ya kwanza leo tangu asajiliwe, Wilbert Mweta, kuwa ndiye aliyefanya uzembe uliozaa bao lililowazamisha.

Mussa Said alipeleka msiba huo Msimbazi baada ya kufunga kwa kichwa goli pekee lililoamua mechi yao ya leo katika dakika ya 73 kufuatia krosi ya Mohammed Jingo.

Milovan alisema baada ya mechi hiyo: "Nimesikitika tumepoteza mchezo, hatukuwa na bahati. Wachezaji walikuwa wamevunjika moyo kutokana na shutuma zinazotolewa na mashabiki dhidi yao baada ya kupoteza mechi ya Mtibwa. Leo Tumepoteza nafasi nyingi za kufunga lakini soka liko hivi. Goli tulilofungwa ni makosa ya kipa."   

Kocha msaidizi wa Toto, Athuman Bilal, alisema: "Timu yetu imecheza vizuri, tulistahili ushindi."

Kipigo kinawaacha mabingwa Simba katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakiwa na pointi 23, moja nyuma ya Azam FC walio katika nafasi ya pili. Mahasimu wao Yanga wanaoongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 26 na watacheza mechi yao kesho dhidi ya timu inayoshika nafasi ya nne ya Coastal Union yenye pointi 22 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kama Coastal itashinda dhidi ya Yanga kesho Simba itakuwa ya nne katika msimamo baada ya mechi 13. 


Azam nayo, ambayo iko katika mgogoro baada ya kuwasimamisha nyota wake kadhaa kwa tuhuma za kupokea rushwa na kuhujumu mechi yao dhidi ya Simba, imebaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 24 baada ya kulala 2-1 dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga leo.
 
Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa;
Simba:
William Mweta, Nasoro Masoud 'Chollo', Paul Ngalema, Komalbil Keita, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa.

Toto Africans:
Erick Ngwengwe, Ally Ahmed, Evarist Maganga, Peter Mutabuzi, Msafiri Hamis, Mussa Said, Emmanuel Swita, Kheri Mohammed, Selemani Kibuta na Mohammed Jingo.

No comments:

Post a Comment