Saturday, November 10, 2012

WALTER CHILAMBO AZOA MIL. 50 ZA EPIQ BSS 2012

Walter Chilambo (wa pili kulia) akibeba sanduku lenye zawadi yake ya fedha taslimu Sh. milioni 50 baada ya kutangazwa mshindi wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la BSS.  Wengine kutoka kushoto ni mshindi wa pili Salma Yusuph, Jaji Mkuu wa Epiq BSS, Madame Ritha, Afisa Biashara Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Simu ya Zantel, Sajid Khan na mabaunsa.

Salutiiiii..... Jaji Master Jay akisimama juu ya meza kuonyesha kumkubali msanii Walter wakati wa fainali ya shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee usiku wa kuamkia leo.

Nyota wa Bongofleva, Ommy Dimpoz (kushoto) akitumbuiza kusindikiza shindano la Epiq BSS wakati wa fainali kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee usiku wa kuamkia leo.

WALTER Chilambo wa jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo alitangazwa kuwa mshindi wa shindano la Epic Bongo Star Search 2012 baada ya kuwashinda wenzake wanne walioingia fainali iliyohitimisha mbio za miezi sita zilizohusisha washiriki zaidi ya 50,000.

Kwa ushindi huo, Walter alizawadiwa Sh. milioni 50 taslimu ambazo alikabidhiwa ukumbini hapo na Afisa Biashara Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Simu ya Zantel, Sajid Khan.

Katika raundi ya kwanza wana fainali hao watano walichujwa wawili ambao ni ndugu, Nsami Nkwabi na Nshoma Ng'hangasamala na kubaki watatu, kabla ya Wababa naye kufuata nje ya mchuano.

Kuaga kwa Wababa ambaye alikuwa akishangiliwa sana huku sehemu ya mashabiki wake wakibeba bango lenye kauli iliyopata kutolewa na Jaji Salama siku za nyuma "Wababa wewe unajua hadi unakera", kulimaanisha kwamba mshindi wa mwaka huu angetoka baina ya kimwana mkali wa kuimba na kupiga gita Salma Yusuph kutoka Zanzibar na Walter.

Lakini alikuwa ni Walter aliyeondoka na zawadi hiyo iliyoboreshwa zaidi mwaka huu kufuatia udhamini mnono wa Zantel.

Walter alifunika kwa wimbo wake wa ni 'Natumaini' wa Beka wa THT, 'Tushukuru Kwa Yote' wa Dogo Ditto na wakati Salma alianza kwa kuimba 'Aifola' wa Linex na 'Gere' ulioimbwa na Nyota Waziri wa bendi ya Njenje.

Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu kampuni na Benchmark Production na wadhamini wake Zantel waliamua kutoa zawadi moja tu kwa mshindi na kutokana na hivyo, washiriki wengine waliobakia wamepata ofa ya kurekodi nyimbo moja kila mmoja katika studio ya Maneke ambaye mwaka huu ndiye alitengazwa kuwa mtengeneza nyimbo bora.

Mkurugenzi wa Benchmark Production, Ritha Poulsen, ambaye ndiye jaji mkuu wa shindano hilo kabla ya kutangazwa kwa mshindi aliwashukuru Watanzania na washiriki wote waliojitokeza kuanzia hatua ya awali kwa kusema kwamba bila wao shindano hilo haliwezi kufanyika.

Alisema anaamini kupitia shindano hilo mshindi anaweza kutimiza ndoto yake na zawadi hiyo itabadilisha maisha yake.

Hata hivyo, mratibu huyo alisema kwamba majaji walikuwa na kazi ngumu ya kuamua mshindi kutokana na vipaji vilivyoonyeshwa na washiriki kuanzia hatua ya kwanza.

"Huu ni mwaka wa sita lakini mwaka huu haikuwa kazi rahisi," alisema Madame Ritha kama anavyojulikana.

Shindano hilo lilipambwa na burudani ya wasanii mbalimbali wakiwamo, Mzee Yusuph aliyeimba kibao chake cha 'Mpenzi Chocolate', Ommy Dimpoz, Mwasiti, Lina, Amin, Ben Pol, Ras Six ambaye alikuwa ni mmoja wa washiriki kwenye hatua za awali na mshindi wa shindano hilo wa mwaka jana ambaye sasa anaimba kwenye bendi ya African Stars, Twanga Pepeta, Haji Ramadhani.

No comments:

Post a Comment