Tuesday, November 13, 2012

RIO FERDINAND ATOSA UAMUZI WA FERGUSON KUMSAJILI TENA SASA NA KUSEMA NI MPAKA KRISMAS NDIPO ATAKAPOAMUA KAMA AENDELEE KUCHEZA MAN U AU LA!

Rio Ferdinand
MANCHESTER, England
RIO Ferdinand ameiambia Manchester United kwamba hana uhakika wa kusaini mkataba mwinine mpya utakaomfanya aendelee kuichezea timu hiyo msimu ujao.

Mkataba wa sasa wa Ferdinand unamalizika katika kipindi kijacho cha usajili wa majira ya kiangazi lakini kocha Alex Ferguson anaamini kwamba beki huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England anaweza kucheza kwa kiwango chake cha juu kwa misimu mingine miwili zaidi na amesema kwamba atapewa ofa ya mkataba wa miezi 12 kuongeza kipindi chake cha kuichezea Man U na kufikia misimu 11.

Hata hivyo, Ferdinand, ambaye alitimiza miaka 34 wiki iliyopita, amekuwa akisumbuliwa mara kwa mara na maumivu ya mgongo katika miaka ya hivi karibuni na atasubiri kwa miezi michache ijayo kabla ya kuamua kama asaini mkataba mwingine utakaomfanya aendelee kucheza ama la.

“Siku zote huwa ni faraja kusikia kocha akizungumza jambo kama hilo, lakini lazima uwe tayari kwa kila wiki na kila mwezi,' Ferdinand aliliambia jarida la Inside United.
“Kitu ninachoweza kufanya ni kusubiri krismasi, na baadaye tena wakati wa majira ya kiangazi kuona ninajisikiaje na kuamua baada ya hapo.

"Lakini kusikia kocha akizungumza namna ile ni wazi kwamba unakuwa umerejeshewa nguvu.

“Nitakuwa na kipindi kizuri cha kuamua ifikapo Desemba au Januari wakati mechi zitakapoanza kuwa nyingi na za haraka. Huo ndio wakati mzuri wa kujua kama uko sawa  na unajua kuwa kazi kweli imeanza.

“Nadhani nitakuwa na kipimno kizuri cha kujua kama kweli niko fiti na baadaye kunufaika na kipindi cha mapumziko ya majira ya kiangazi.”

Itakuwa ni jambo la kushangaza ikiwa Ferdinand ataamua kutundika viatu vyake, na vyanzo kutoka ndani ya Man U vinaamini kwamba atashawishiwa ili aendelee kucheza.
Beki huyo wa zamani wa West Ham na Leeds amekuwa mhimili katika safu ya mabeki wa Man U msimu huu baada ya kukosekana kwa Nemanja Vidic, Chris Smalling na Phil Jones, akicheza mechi 11 za klabu yake kati ya 15 za Ligi Kuu ya England na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

No comments:

Post a Comment