Wednesday, November 14, 2012

RAIS KIKWETE AWATOLEA UVIVU CCM KWA KUWAAMBIA KAMWE WASITEGEMEE POLISI KUJIBU MAPIGO YA WAPINZANI... AWAAMBIA WAKITUMAINIA NGUVU ZA POLISI TU, BASI WAJUE CHAMA KINAKUFA... AKUMBUSHIA NAMNA DK. SLAA ALIVYOMZULIA UONGO KUWA ETI ALIJICHIMBIA HOTELI YA LA KAIRO MWANZA WAKIPANGA NJAMA MBAYA AKIWA NA MWANAWE RIDHIWANI KIKWETE, EDWARD LOWASSA NA ROSTAM AZIZ WAKATI UKWELI NI KWAMBA SIKU ILIYOTAJWA YEYE ALIKUWA JIMBO LA MTAMA MKOANI LINDI, AKALALA HUKO NA KUAMKIA HUKO HUKO LINDI... !

Rais Kikwete (katikati) akiongoza mkutano mkuu wa CCM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  Jakaya Mirsho Kikwete, amewatolea uvivu viongozi na wanachama wenzake wa CCM kwa kuwaambia kuwa kamwe wasitarajie kutumia nguvu za Jeshi la Polisi kudhibiti wapinzani kwani kwa kufanya hivyo watakiua chama chao.

Akizungumza wakati akihutubia wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kabla ya kuufunga leo usiku (Novemba 13, 2012), Kikwete alisema kuwa kamwe CCM haitadumu kama viongozi na wanachama wake watategemea nguvu za polisi kukabiliana na 'uongo' unaosambazwa na viongozi wa vyama vya upinzani dhidi ya chama tawala na kwamba, kamwe polisi hawawezi kusaidia chama chao katika kukabiliana na 'uongo' wa wapinzani.

Badala yake, Kikwete aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa wanachama wa CCM wanapaswa kujibu mapigo ya wapinzani kwenye majukwaa ya kisiasa, kwa kueleza ukweli wa mambo na kufuta uongo wa wapinzani ambao ukiachwa bila kujibiwa, unaweza kuzoeleka na kuchukuliwa kuwa ni kweli.

"Hivi wapinzani wakisema kuwa Kikwete nchi imemshinda mtataka polisi  waende kuwakamata...! Hapana... mnachotakiwa ni kujibu kwa kueleza mazuri tunayofanya," alisema Kikwete.

Aliongeza kuwa baadhi ya watu wana CCM wamekuwa wakija juu kila mara wanaposikia uongo wa wapinzani na kuhoji kulioni serikali inatulia tu na kuwaacha; fikra ambazo si sahihi kwani kutumia polisi hakufuti uongo unaosambazwa na wapinzani bali ni kwa kujibu mapigo kwenye majukwaa ya kisiasa na kueleza ukweli.

AMTUHUMU DK. SLAA

Akitolea mfano, Rais Kikwete alisema kuwa kuna siku wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, Dk. (Wilbroad) Slaa aliudanganya umma kwa kudai kuwa eti, yeye (Kikwte), mwanawe Ridhiwani Kikwete, Edward Lowassa na Rostam Aziz walijichimbia katika hoteli ya La Kairo jijini Mwanza kupanga njama mbaya.

Kikwete akasema huo ulikuwa ni uongo mkubwa kwani hata katika siku hiyo iliyotajwa na Slaa, yeye alikuwa katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi ambako alilala na kuamkia huko huko Lindi.

Akasema kuwa taarifa kama hizo zinatakiwa kujibiwa na wana CCM na siyo kuziacha kwa kutegemea polisi waingilier kati, au kulalamika tu kwa kusema: "Ndiyo walivyo hawa... tumeshawazoea!"

ASHINDA KWA ASILIMIA 99.92

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alitangazwa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa kipindi cha miaka mingine mitano baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama chake kumpa ushindi wa asilimia 99.92.

Akitangaza matokeo ya kura hizo, Spika wa Bunge aliyekuwa msimamizi mkuu alisema kuwa kura zilizopigwa ni 2,397 na Kikwete alizoa kura 2,395 huku kukiwa hakuna kura hata moja iliyoharibika.

Mbali na Kikwete, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Philip Mangula alichaguliwa kwa kishindo pia kuwa  Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara baada ya kupata kura zote 2,397 (asilimia 100), sawa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein aliyechaguliwa kwa kishindo pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM visiwani Zanzibar baada ya kupata kura zote za ndiyo kati ya 2,397 zilizopigwa na hakuna iliyoharibika.

Mangula anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Pius Msekwa aliyepumzishwa kutokana na umri huku Shein akitwaa nafasi iliyoachwa na rais mstaafu wa Zanzibar, Amaan Abeid Karume.

Mkutano huo mkuu wa nane CCM umefungwa usiku huu na Rais Kikwete na unatarajiwa kufanyika tena Agosti, 2015.

No comments:

Post a Comment