Wednesday, November 14, 2012

MESSI AMPIKU CRISTIANO RONALDO NA KUTWAA TUZO YA MWANASOKA BORA WA LA LIGA 2011/2012... IKER CASILAS AMBWAGA VICTOR VALDES TUZO YA KIPA BORA... SERGIO RAMOS AWAGARAGAZA KINA GERARD PIQUE TUZO YA BEKI BORA... INIESTA AMSHINDA MESUT OZIL TUZO YA KIUNGO MSHAMBULIAJI BORA...XABI ALONSO AMTESA SERGIO BUSQUETS TUZO YA KIUNGO MKABAJI BORA NA PEP GUARDIOLA AMBWAGA JOSE MOURINHO TUZO YA KOCHA BORA WA LA LIGA 2011/12

Lionel Messi 
BARCELONA, Hispania
STRAIKA wa Barcelona, Lionel Messi ametangazwa kuwa Mwanasoka Bora wa msimu uliopita wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania 2011-02, akiwapiku wapinzani wake wawili wanaotoka katika klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo na Karim Benzema.

Messi, ambaye alifunga magoli 50 katika La Liga msimu uliopita, alitajwa vilevile kuwa mshindi wa tuzo ya Straika Bora wa msimu wakati kocha wake wa zamani, Pep Guardiola alichaguliwa kuwa Kocha Bora katika kura zilizopigwa na wachezaji na makocha wa ligi mbili za juu nchini Hispania, akiwashinda makocha kadhaa akiwamo Jose Mourinho wa Real Madrid.

“Nataka niwashukuru makocha walionichagua kuwa Mwanasoka Bora na wachezaji wenzangu ambao pia wamenichagua kuwa Mwanasoka Bora. Nina furaha kubwa na, ninajivunia sana tuzo hii,” amesema Messi baada ya kushinda tuzo hizo mbili kwa mwaka wa nne mfululizo.

Katika msimu wake wa mwisho akiwa Barcelona, Guardiola aliiongoza Barcelona kutwaa Kombe la Mfalme, taji la Hispania la Super Copa, taji la Ulaya la Super Super Cup na Kombe la FIFA la Klabu Bingwa Dunia. Timu hiyo pia ilimaliza ya pili kwenye msimamo wa La Liga na kufika nusu fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Wakati huo huo, Andres Iniesta alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Kiungo Mshambuliaji Bora na kuwashinda Ozil wa Real Madrid na Santi Carzola aliyekuwa Malaga (sasa Arsenal), Carlos Puyol akatwaa tuzo ya Nidhamu na yosso wa kikosi cha Barcelona B, Marc Bartra alishinda tuzo ya kuwa Beki Bora wa Ligi Darajala Pili.

Real Madrid, ambayo ilihitimisha ubabe wa Barcelona wa kutwaa ubingwa wa La Liga mara tatu mfululizo, pia walitwaa baadhi ya tuzo zikiwamo za Iker Casillas kuwa Kipa Bora, Sergio Ramos akawa Beki Bora na kuwashinda kina Gerard Pique (wa Barca), na Xabi Alonso akatwaa tuzo ya Kiungo Mkabaji Bora, akimshinda  Sergio Busquets wa Barca.

“Napenda kuwashukuru makocha walionichagua kuwa Kipa Bora msimu uliopita,” amesema Casillas, aliyemshinda kipa wa Barcelona, Victor Valdes na kipa wa Real Zaragoza, Roberto.

“Nimefurahishwa na ushindi huu na, natumai kuwa nitashinda tena mwakani, hivyo kuwa mara ya tatu kwangu.”

Yosso wa Malaga, Isco alishinda tuzo ya kuwa Mchezaji Bora Anayeinukia wakati tuzo ya Mchezaji Bora wa Daraja la Pili imetua kwa veterani wa Deportivo La Coruna aliyeisaidia timu hiyo kurejea katika ligi kuu, Juan Carlos Valeron.

No comments:

Post a Comment