Natishaaa...! Peter
Odemwingie akishangilia goli alilofunga dhidi ya Southampton
wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England mjini West Bromwich, jana Novemba 5,
2012.
|
Peter
Odemwingie wa West Bromwich Albion (kulia) akifunga goli dhidi ya Southampton
wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England mjini West Bromwich, jana Novemba 5,
2012.
|
LONDON, England
PETER Odemwingie alifunga mara
mbili kuisaidia West Bromwich Albion kuendeleza mwanzo wao mzuri msimu huu kwa
ushindi wa 2-0 dhidi ya timu inayoburuta mkia ya Southampton na kukwea hadi
katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England jana.
Shuti la mshambuliaji Odemwingie
katika dakika ya 36 lilifungua akaunti ya magoli ya wenyeji na Mnigeria huyo
akaongeza jingine katika dakika ya 60 baada ya kuunganisha vyema kwa kichwa cha
karibu na lango krosi ‘kali’ ya Shane Long.
West Brom wana pointi 17 kutokana
na mechi 10, sawa na timu inayokamata nafasi ya nne ya Everton na saba nyuma ya
vinara Manchester United.
Southampton wamejikusanyia pointi
nne, sawa na Queens Park Rangers ambayo haijawahi kushinda, lakini wako mkiani
mwa msimamo wa ligi kutokana na tofauti ya mabao.
West Brom wamepoteza pointi
katiika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya mabingwa Manchester City na pia Newcastle
United, kwa kuruhusu magoli ya dakika za majeruhi lakini safari hii hawakufanya
makosa dhidi ya kikosi cha Southampton.
Zoltan Gera alipoteza nafasi ya
wazi katika dakika ya 20 wakati shuti la Odemwingie lilipokwenda moja kwa moja
miguuni mwake lakini akiwa umbali wa yadi sita kutoka golini akapiga shuti
lililopaa juu ya lango.
Baada ya goli la utangulizi la Odemwingie
lililotokana na shuti lililomparaza Maya Yoshida na kumpita kipa Paulo
Gazzaniga, Southampton walikosa bahati ya kusawazisha baada ya shuti la Rickie
Lambert kugonga ‘besela’ mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Kipa wa West Brom, Ben Foster alifanya
kazi nzuri ya kuokoa na kuinyima Southampton goli katika muda wa majeruhi.
Odemwingie alifurahishwa na
kiwango cha timu yake baada ya kupata vipigo katika dakika za majeruhi kutoka
kwa Man City na Newcastle.
"Haya yalikuwa majibu mazuri
kutoka kwa timu nzuri. Tulihitaji bahati kidogo na ni rahisi, kama mkiendelea
kupiga mashuti mtafunga, tumefurahi kupata pointi zote tatu," Odemwingie aliiambia
Sky Sports.
No comments:
Post a Comment