Rais Kikwete akimjulia hali Sheikh Soraga aliyelazwa ICU kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili leo Novemba 6, 2012.. |
Pole Sheikh sana...! Rais Kikwete akimjulia hali Sheikh Soraga aliyelazwa ICU kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili leo Novemba 6, 2012. |
Mbebe kwa uangalifu... Sheikh Soraga akibebwa kuwahishwa Muhimbili. |
Harakati za kumuwahisha Sheikh Soraga Muhimbili akitokea Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar. |
Hapa Sheikh Soraga akianza kutolewa na gari la wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar kupelekwa Uwanja wa Ndege kabla ya kukimbiziwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili. |
Katibu
wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga amelazwa ICU katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es
Salaam akiwa hoi baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana katika eneo
la Magogoni Msumbiji Mkoa wa Mjini Magharibi mjini Zanzibar leo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amekwenda kumpa pole
Sheikh Soraga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kumtakia kheri ili apone
haraka.
Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai,Yussuf Ilembo, amesema wakati akizungumza na waandishi
wa habari kwenye makao makuu ya Jeshi la
Polisi, Ziwani Zanzibar kuwa Sheikh Soraga ameimwagiwa tindikali leo alfajiri wakati
akifanya mazoezi binafsi ya viungo.
Ilembo
alisema wakati akiendelea na mazoezi, alimuona mtu mwingine akifanya mazoezi mbele
yake kabla mtu huyo hajamgeukia na kumwagia tindikali iliyomjeruhi vibaya sehemu
za usoni na kifuani.
Baadaye
mtu aliyefanya unyama huo alitoweka na kuelekea kusikojulikana.
Ilembe
alisema tayari uchunguzi umeanza kufanyika na Jeshi la Polisi litahakikisha
linatumia nguvu zake zote kuwasaka wahusika.
Sheikh
Soraga alifikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar lakini baadaye,
kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa
Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Dk. Jamala Adam Taib, walilazimika kumkimbizia jijini
Dar es Salaam ambako alipelekwa kwa ndege iliyotolewa na serikali na kufikishwa katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
Wakati
akisafirishwa kutoka Zanzibar, Sheikh Soraga alibebwa katika gari la wagonjwa
aina ya Toyota (Na. DFP 5049), kisha akapakiwa
katika ndege ya serikali yenye namba 5H-TGF Tanzania, mishale ya saa 3:45
asubuhi kupelekwa Dar es Salaam na kusindikizwa na viongozi mbalimbali, akiwamo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali iddi.
Mufti
wa Zanzibar, Sheikh Saleh Kabi, aliwataka wananchi kuwa na subira kufuatia
tukio hilo.
Alisema
Zanzibar inaweza kuingia katika maafa makubwa iwapo watu watapoteza subira na uadilifu
na kwamba wasipokuwa makini, wanaweza kujitumbukiza katika maafa makubwa kama
ilivyokuwa katika nchi nyingine barani Afrika kama Rwanda.
Vyama
vya CCM na CUF vinavyoongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar cimelaani
vikali tukio hilo na kutaka uchunguzi mkali ufanywe ili wahusika wafikishwe
mbele ya mkono wa sheria.
“Tunawaomba
wananchi watoe ushirikiano kwa polisi ili kuwafichua watu wanaohusika na iovu
kama huu,” amesema Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Zanzibar, Salim Bimani.
No comments:
Post a Comment