Luteni Yusuf Rajab Makamba |
Akizungumza leo jioni wakati akimpigia debe rais Jakaya Kikwete mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kumchagua kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka mingine mitano, Makamba alisema kuwa Yanga, timu asiyoishabikia kwa vile yeye ni mwanachama wa Simba na pia Coastal Union anapokuwa kwao jijini Tanga, ilifanya vizuri kwa kusajili wachezaji wenye sifa; lakini 'ikachemka' kwa kuteua kocha asiyewafaa (Tom Saintfiet) na matokeo yake wakajikuta wakipata matokeo mabovu mwanzoni mwa msimu.
"Yanga chini ya mwenyekiti ambaye ni rafiki yangu Yusuf Manji, wakawa wajanja kwa kujua kuwa kocha hawafai na wakambadili mara moja... na sasa wanapata matokeo mazuri na kuiburuza Simba," alisema Makamba na kushangiliwa na wajumbe wa NEC wa CCM.
Makamba alitoa mfano huo wakati aklielezea umuhimu wa kocha katika timu ya soka; akilinganisha ubora wa kiwango cha juu wa 'kocha' Jakaya Kikwete kwa chama chao cha CCM, akitaka wajumbe wampigie kura nyingi za ndiyo ili aendelee kukiongoza chama chao kwa mafanikio makubwa.
Yanga walianza vibaya mwanzoni mwa msimu kwa kushikiliwa kwa sare ya 0-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya na baadaye wakala kipigo cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar na baada ya hapo, uongozi ukamtimua kocha kutoka Ubelgiji, Tom Saintfiet na nafasi yake wakampa Mholanzi Brandts ambaye sasa anaendelea kuipa mafanikio timu hiyo inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kuwa na pointi 29 na kufuatiwa na Azam yenye pointi 24 huku mahasimu wao wa jadi, Simba wakishika nafasi ya tatu kwa kubaki na pointi zao 23 baada ya kumalizika kwa mechi zote 13 za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment