Thursday, November 22, 2012

MUME CHAPOMBE AWAUA MKEWE NA MTOTO WAKE KWA KUWANYONGA SHINGONI ETI KISA KANYIMWA SENTI ZA KWENDA KUFAKAMIA MIPOMBE... POLISI WAMTIA MBARONI

Kaimu Kamanda wa Polisi jijini Mwanza, Lilian Matola.
Mkazi wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Paul Zalia (36), amemuua mke wake na mtoto wao wa miaka miwili kwa kuwanyonga shingoni.

Tukio hilo la kikatili lilitokea usiku wiki iliyopita, nyumbani kwa mtuhumiwa katika kijiji cha Kagogoro, kilichopo kisiwa cha Meisome.

Habari zinasema kuwa, chanzo cha mauaji hayo ni mtuhumiwa Zalia kumuomba fedha mkewe kwa ajili ya kununulia pombe na marehemu kumnyima fedha hizo.

Diwani wa eneo hilo, Mtanzania Mazabari, alimtaja marehemu kuwa ni Muleba Magesa (30) na mwanae mwenye umri wa miaka miwili, ambaye hata hivyo jina lake halikutajwa.

Inadaiwa kuwa, mtuhumiwa ambaye anashilikiwa na Polisi, kabla ya tukio hilo alikuwa na ugomvi na mke wake kwa zaidi ya siku mbili akimtaka ampatie fedha alizopata kutokana na mchezo wa kuchangiana fedha na wanawake wenzake (upatu) ili akazitumie kunywea pombe.

Hata hivyo, habari hizo zinasema kuwa marehemu alikataa amri ya mme wake na baada ya kulumbana kwa zaidi ya siku mbili ndipo mtuhumiwa alipowavizia marehemu na mwanaye usiku wa manane wakiwa wamelala na kuwanyonga hadi kufa.

Diwani huyo alisema kuwa mtuhumiwa alikutwa akiwa katika harakati za kutaka kutoroka baada ya kutenda tukio hilo la kinyama, lakini wananchi walifanikiwa kumtia nguvuni na kumfikisha katika kituo cha polisi.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Sengerema (OCD), Prudencia Protace, alithibitisha kutokea tukio hilo na kwamba mtuhumiwa anashikiliwa katika kituo cha Butandwa wilayani hapa.

Kifo cha marehemu hao kilithibitishwa pia na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Meisome, Peter Ogecho, ambaye alifafanua kuwa uchunguzi umebaini kuwa marehemu waliuawa kwa kunyongwa shingo.

Ogecho alisema kuwa baada ya kuifanyia uchunguzi miili ya marehemu, alibaini kwamba walifariki kutokana na kunyongwa shingo.

Tukio hilo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho.

Marehemu walizikwa jana huku Jeshi la Polisi likisema kuwa  mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu mashitaka ya mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment