Thursday, November 22, 2012

WANAJESHI 10 WA JWTZ WATUPWA MBARONI KWA MAUAJI YA RAIA MBEYA, KUJERUHI WENGINE SITA... WALIVAMIA BAA NA KUTEMBEZA KICHAPO KWA KILA WALIYEKUTANA NAYE NA KUZUA BALAA KUBWA...! TUKIO HILI LAIBUKA IKIWA NI SIKU MOJA TU BAADA YA WANAJESHI WENGINE WATATU KUHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA KWA KUKUTWA NA HATIA YA KUMUUA MTOTO WA CHIFU FUNDIKIRA...!

Mkuu wa majeshi nchini, Jenerali Davis Mwamnyange

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Vuai Nahodha
Siku moja tu baada ya wanajeshi watatu kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa na Jaji Zainab Miruke wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa kukutwa na hatia ya kumuua raia Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa marehemu Chifu Fundikira, wanajeshi wengine wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wametiwa mbaroni jijini Mbeya wakidaiwa kuvamia baa na kutembeza kipigo kikali kwa raia kabla ya kusababisha kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi vibaya raia wengine sita.
Wanajeshi hao 10 wa JWTZ wanaoshikiliwa na Polisi jijini Mbeya ni wa Kikosi cha 44 KJ, kambi ya mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya.

Raia aliyeuawa ametajwa kuwa ni Petro Sanga (25), ambaye anadaiwa kufariki dunia baada ya askari hao kumchoma kisu shingoni na mdomoni.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, amethibitisha juu ya kushikiliwa polisi kwa wanajeshi hao kuhusiana na tukio hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,  Diwani Athumani, askari hao wanatuhumiwa kumuua kijana huyo Novemba 18, mwaka huu, saa 3.00 usiku, wakati akinywa pombe katika baa ya Power Night Club, iliyoko Mbeya.

Kamanda Athumani alisema kabla ya mauaji hayo, kijana huyo wakati akinywa kwenye baa hiyo wanajeshi hao walivamia na kuanza kuwashambulia kwa kipigo wananchi waliowakuta.

Alisema kuwa askari hao walimshambulia kijana huyo kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake kwa mateke, mikanda, marungu, sime na mapanga kisha kumchoma kisu.

“Wakati watuhumiwa hao wakimshambulia, kijana huyu alijaribu kujinasua kwa kukimbilia kwenye baa ya Vavenemwe,” alisema Kamanda Athumani.

Alisema kutokana na kipigo hicho, kijana huyo alipoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Mbeya Vijijini ya Ifisi, iliyopo katika mji mdogo wa Mbalizi.

Kamanda Athumani alisema kijana huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kutokana na majeraha na kutoka damu nyingi.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya polisi kupata taarifa, walikwenda eneo la tukio.

Kamanda huyo alisema katika uchunguzi wao, waligundua kuwa askari hao waliwashambulia wananchi hao na kuumua kijana huyo kulipiza kisasi baada ya askari mwenzao, Godfrey Matete (30), kushambuliwa.

Alisema Matete alishambuliwa na walinzi wa klabu ya pombe za kienyeji maarufu kwa jina la DDC, Novemba 17, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, polisi wanawashikilia walinzi wanne wa klabu hiyo kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kumshambulia mwanajeshi huyo.

Aliwataja walinzi hao ambao ni wakazi wa Izumbwe wilayani humo kuwa ni Frank Mtasimwa (25), Mure Julius (26), Omari Charles (28) na Reginald Mwampete.

Hata hivyo, Kamanda Athumani hakuwa tayari kutaja majina ya wanajeshi hao waliokamatwa kwa madai kuwa uchunguzi dhidi yao bado unaendelea.

“Majina ya watuhumiwa yatatajwa baadaye kwa sababu bado uchunguzi unaendelea,” alisema Kamanda Athumani.

Alisema uchunguzi ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kufanya vurugu na kusababisha mauaji ya kijana huyo.

Aliwashauri watumishi wa vyombo vya dola kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa kunasababisha madhara kwa jamii na uharibifu wa mali kama magari kuvunjwa vioo.

Akizungumza jana jioni baada ya kupigiwa simu ili kuzungumzia suala hilo, msemaji wa JWTZ, Kanali Mgawe alisema muda huo alikuwa nje ya kituo cha kazi.

Hata hivyo, alisema kuwa alipigiwa simu na baadhi ya waandishi wa habari wakiulizia kuhusu taarifa za kukamatwa kwa askari hao.

“Baada ya kupigiwa simu na waandishi, nilipiga simu kambini kuulizia wakaniambia ni kweli kuna askari wetu wamekamatwa, wanashikiliwa, wako mahabusu Mbeya,” alisema Kanali Mgawe.

Hata hivyo, alisema hana taarifa zaidi kuhusiana na kukamatwa kwa askari hao.

Juzi, wanajeshi Mohamed Rashid, Ali Ngumbe na Sajenti Rhoda walihukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahkaam Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Swetu Fundikira saa 7:00 usiku, katika barabara ya Mwinjuma, eneo  la Kinondoni jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment