Thursday, November 1, 2012

MOTO WA KINA HAZARD, RAMIRES, STURRIDGE WAISAIDIA CHELSEA KUIKANDAMIZA MAN U 5-4... LIVERPOOL WACHAPWA 3-1 NA SWANSEA

Hazard akishangilia goli alilowatungua Man U kwa penati katika mechi yao ya Kombe la Capital One jana usiku Oktoba 31, 2012. (Picha: Reuters)
Wewwweeeeee....! Hazard akishangilia
Ryan Giggs wa Man U (kulia) akifunga goli lao la ufunguzi dhidi ya Chelsea katika mechi yao ya raundi ya nne ya Kombe la Capital One kwenye Uwnaja wa Stamford Bridge jana usiku Oktoba 31, 2012. (Picha: Reuters)
Sturidge (aliyebebwa) akishangilia goli alilofunga dhidi ya Man na wachezaji wenzake Ramires na Hazard katika mechi yao ya Kombe la Capital One kwenye Uwanja wa Stamford Bridge jana usiku. 
Edin Hazard
Nani (kulia) wa Man U (kulia) akipongezwa na mwenzake Anderson baada ya kufunga goli dhid ya Chelsea katika mechi yao ya kuwania Kombe la Capital One jana usiku. (Picha: Reuters)
Nathan Dyer wa Swansea City (katikati) akibanwa na Jack Robinson na Luis Suarez wa Liverpool wakati wa mechi yao ya raundi ya nne ya Kombe la Capital One kwenye Uwanja wa Anfield jana usiku Oktoba 31, 2012 mjini Liverpool, England. Swansea ilishinda 3-1 (Picha: Reuters)
Aiya weeee....! Luis Suarez wa Liverpool akisikitika baada ya timu yake kula kichapo katika mechi yao ya raundi ya nne ya Kombe la Capital One dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Anfield jana usiku Oktoba 31, 2012. (Picha: Reuters)

LONDON, England
WASHAMBULIAJI wa Chelsea walikuwa juu mno jana usiku dhidi ya beki ‘yosso’ wa Manchester United wakati wenyeji waliposhinda kwa mabao 5-4 na kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Capital One watakayocheza dhidi ya Leeds United.

Chelsea walifanya makosa mawili kwenye safu yao ya mabeki wakati Ryan Giggs na Javier Hernandez walipofunga kila mmoja huku goli la kwanza la kusawasisha la wenyeji likiwekwa wavuni kwa njia ya penati na David Luiz.

Gary Cahill alifanya ubao wa magoli usomeke 2-2 lakini goli jingine la Man U kutokana na mpira wa kubetua wa Nani lilionekana lingemaliza mechi, kabla ya kusawazishwa kupitia penati ya Eden Hazard.

Daniel Sturridge na Ramires walifunga kila mmoja katika dakika 30 za nyongeza kabla Giggs hajaifungia Man U goli la nne kwa njia ya penati.

Luiz pia aligongesha ‘besela’ katika nusu saa iliyoongezwa wakati Chelsea ilipomaliza mechi hiyo ikiwa kidedea na kustahili ushindi baada ya kuwaingiza nyota wao walioanzia benchi.

Lakini pia walimshukuru beki yosso wa kati wa Man U, Scott Wootton, aliyemsukumiza Ramires kuwazawadia Chelsea penati ya pili katika dakika za majeruhi na baadaye akapiga pasi fupi ya kichwa kumrudishia kipa Anders Lindegaard ambayo mwishowe ilinaswa na Sturridge na kuwapa wenyeji goli jingine muhimu.

Mechi hiyo ya kusisimua ilistahili hasa kumaliza ‘bifu’ lililotokana na mechi yao ya Ligi Kuu ya England siku tatu zilizopita, wakati refa Mark Clattenburg alipowatoa nje kwa kadi nyekundu wachezaji wawili wa Chelsea na kutuhumiwa kutumia “lugha chafu” dhidi ya John Mikel Obi na Juan Mata.

Refa Lee Mason alichezesha vizuri sana juzi, akitoa penati zote tatu kwa usahihi na pia kushughulikia vyema ugomvi kati ya Oscar na Nani ulioonekana kutaka kuharibu.

Baada ya kuongoza katika nusu ya kwanza, Man U walijikuta wakigeuziwa kibao wakati Hazard na Oscar walipoungana na Mata, Moses na Sturridge katika kuunda safu ya ushambuliaji yenye nyota watano wa Chelsea baada ya mapumziko.

Lakini kabla ya mapumziko, kikosi cha kocha Alex Ferguson kilionekana kujipanga vyema, huku Chelsea wakinaswa mara mbili wakati wakicheza nje ya eneo lao, kipa Petr Cech na David Luiz wote wakistahili kubeba lawama.

Goli la utangulizi la Man U lilipatikana wakati Cech alipomuanzishia mpira Oriol Romeu aliyekuwa peke yake karibu na eneo la penati, lakini Anderson aliuwahi mpira, akampasia Giggs kabla winga huyo mwenye miaka 38 kutofanya makosa na kumalizia vyema kwa kuupeleka mpira huo wavuni, pembeni kwa chini ya lango.

Hadi kufikia wakati huo wageni walikuwa wamepiga mashuti mengi yaliyolenga lango lakini hakukuwa na hata moja kali la kumsumbua Cech, wakati safu ya kiungo iliyokuwa na wazoefu Giggs, Darren Fletcher na Anderson ikimlinda kirahisi beki yosso wa kati wa kikosi chao ambacho kilimshuhudia kocha Alex Ferguson akibadili wachezaji 10 kulinganisha na kikosi kilichoanza katika mechi yao ya Jumapili.

Hata hivyo, mmoja kati ya wachezaji wenye sura mpya kikosini, Alexander Buttner, alimuangusha Moses na kuipa Chelsea penati ya kwanza iliyofungwa na Luiz.

Mbrazili huyo alipiga penati ‘kali’ lakini ndiye aliyehusika na goli la pili la Man U wakati alipokokota mpira kuvuka nusu ya uwanja na kunyangan’nywa na Mbrazili mwenzake, Rafael.

Anderson aliinasa pasi aliyopewa na kumpenyezea Javier Hernandez “Chicharito” aliyemfunga Cech kwa mara ya sita katika mechi tisa alizocheza dhidi ya Chelsea.

Rafael, mchezaji pekee aliyekuwamo pia katika kikosi cha Man U kilichocheza Jumapili, alihamia kwenye nafasi ya beki wa kushoto katika kipindi cha pili na ndiye aliyemnyang’anya mpira Sturridge kabla ya kufunga goli la kusawazisha, lakini beki huyo wa pembeni wa Man U alishindwa kumzuia Cahill wakati akiwahi kona ya Mata na kufunga goli lililofanya matokeo yawe 2-2.

Dakika saba baadaye, Nani aligongeana vyema pasi za ‘one-two’ na Anderson kabla ya kufunga na kuipa Man U uongozi kwa maa nyingine tena.

Wootton alimsukuma Ramires na kusababisha penati iliyowekwa wavuni na Hazard na mwishowe, Sturridge akatumia vyema makosa mengine ya Wootton aliyepiga pasi ya kichwa chepesi kumrudishia Lindegaard na mahsambuliaji huyo akauwahi mpira na kuipa Chelsea uongozi.

Hazard alimtengenezea pasi safi Ramires aliyefunga na kufanya matokeo yawe 5-3 na hivyo, hata baada ya Giggs kuongeza bao jingine la penati baada ya Chicharito kuangushwa, bado Chelsea walitoka kifua mbele kwa ushindi wa 5-4.

Katika mechi nyingine za Kombe la Capital One jana, Swansea City walishinda 3-1 dhidi ya Liverpool na Norwich waklshinda 2-1 dhidi ya Tottenham. 

Katika hatua ya robo fainali, Bradford watavaana na Arsenal, Leeds United dhidi ya Chelsea, Norwich City dhidi ya Aston Villa na Swansea watacheza dhidi ya Middlesbrough.

No comments:

Post a Comment