Thursday, November 1, 2012

ABDALLAH MAJURA BULEMBO ASHINDA UENYEKITI WA TAIFA WAZAZI CCM... NI REFA WA ZAMANI WA SOKA NCHINI 'ALIYEWAGARAGAZA' VIBAYA JOHN BARONGO NA MHESHIMIWA MBUNGE VITI MAALUM (CCM) MARTHA MLACHA...!

Nitashinda tu... ! Hapa ni siku ambayo Bulembo alikuwa akitangaza nia yake ya kugombea uenyekiti wa Jumuiya  ya Wazzi CCM. 
Pokea fomu yangu...! Bulembo (kushoto) akikabidhi fomu yake ya kugombea uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM.  
Refa wa zamani wa soka aliyewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara, Abdallah Majura Bulembo, ameibuka kidedea na kuwa mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM taifa baada ya kuzoa kura nyingi na kuwaacha mbali wapinzani wake John Barongo na Martha Mlacha ambaye ni Mbunge wa Viti maalum kupitia chama hicho.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo jana, msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma, Steven Wassira 'Tyson', alisema Bulembo ameshinda na sasa ndiye mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Wazazi CCM kwa kipindi kijacho cha miaka minne baada ya kuzoa kura 680 na kuwabwaga wagombea wengine wote.

Alisema kuwa Martha Mlata alipata kura 190 na hivyo kumaliza katika nafasi ya pili huku  John Barongo akiambulia kura 42 tu na hivyo kuwa nyuma ya Bulembo na Mlata.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuibuka mshindi na kutangazwa rasmi kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Bulembo aliyekuwa akishangiliwa ukumbini mfululizo aliwashukuru wajumbe kwa kumpa ushindi wa kishindo, lakini akawaasa baadhi ya watu walioshindwa kwenye uchaguzi huo kukubaliana na matokeo ili kuendelea kukijenga chama chao.

"Miaka minne iliyopita nilisimama pia mbele yenu hna kuwaomba kura, lakini nikashindwa kwa vile kura hazikutosha... hata hivyo niliwashukuru sana na kuahidi kurudi. Leo nimetimiza wajibu huo. Lakini nasikitika kuona wenzangu ambao hawakusimama hapa," alisema Bulembo.

"Kura zao hazikutosha, hawakusaini, wamekimbia, wanaanzisha ajenda mpya... nawakumbusha kuwa katika Chama cha Mapinduzi (CCM) kuna kushinda na kushindwa. Wakubali matokeo kama mimi nilivyofanya miaka minne iliyopita," alisema Bulembo ambaye katika uchaguzi uliopita alishika nafasi ya pili baada ya kuzidiwa kura na Balozi Athumani Juma Mhina aliyetwaa nafasi ya uenyekiti lakini sasa ni marehemu, 

Wengine waliofanya vizuri katika uchaguzi huo ni pamoja na Pandu Silima na Haji waliotwaa nafasi za ujumbe wa NEC-CCM kutokea Zanzibar huku wagombea wengine watatu wakiwamo Mussa Azzan Zungu na Adam Malima wakitwaa nafasi ya ujumbe wa NEC-CCM kutokea Tanzania Bara.

Mbali na kuwahi kuwa refa na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara (MRFA), Bulembo pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

No comments:

Post a Comment