Tuesday, November 6, 2012

MAN UNITED KUWEKA SANAMU YA KOCHA ALEX FERGUSON KWENYE UWANJA WA OLD TRAFFORD

Alex Ferguson

 
LONDON, England
MANCHESTER United watasherehekea miaka 26 ya uongozi wa kocha Alex Ferguson katika klabu yao kwa kumjengea sanamu mwezi huu, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England ilisema katika taarifa yake leo.

Sanamu hiyo itatambulishwa rasmi kwenye Uwanja wa Old Trafford Novemba 23, siku moja kabla Man U hawajacheza dhidi ya Queens Park Rangers, wapinzani hao hao ambao kocha huyo mwenye miaka 70 alikumbana nao katika mechi yake ya kwanza ya nyumbani akiwa na klabu hiyo Novemba 22, 1986.

Ferguson ndiye kocha wa klabu ya soka mwenye mafanikio makubwa zaidi nchini England baada ya kuiongoza Man U kutwaa mataji 12 ya Ligi Kuu, mawili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, matano ya Kombe la FA na manne ya Kombe la Ligi.

Kabla ya hapo alikuwa akiifundisha Aberdeen ya Scotland na kutwaa Kombe la Washindi la Ulaya mwaka 1983 baada ya kushinda katika fainali dhidi ya Real Madrid ya Hispania.

Sanamu hiyo itawekwa karibu na sehehmu ya kuingilia kwenye jukwaa lililopewa jina la kumuenzi Ferguson mwaka jana.
No comments:

Post a Comment