PARIS, Ufaransa
Ndugu wawili, Andre Ayew na Jordan Ayew walifunga kila mmoja wakati Olympique Marseille ilipokwea kileleni na kuungana na Paris St Germain ya kina Zlatan Ibrahimovic kuongoza Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya AC Ajaccio.
Andre alifunga goli la utangulizi katika dakika ya 10 ya kipindi cha pili.
Mdogo wake na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ghana, straika Jordan Ayew, aliongeza la pili dakika tatu kabla ya mechi kumalizika wakati Marseille ikiifikia PSG kwa kuwa na pointi 22, wakizidiwa kwa tofauti ya mabao na hivyo kuwa katika nafasi ya pili.
Hata hivyo, Marseille badi wana mechi moja mkononi watakayocheza nyumbani na hivyo kuwa na nafasi ya kuiacha PSG iliyochapwa 2-1 katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya St Etienne .
Wakati Andre na Jordan waking'ara kwa kuifungia magoli ya ushindi Marseille jana, baba yao Abedi Pele alikuwa jijini Dar es Salaam ambako alitoka kuwapa nasaha nzito wachezaji wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) na baadaye akawa miongoni mwa mashuhuda wa mechi ya Ligi Kuu kati ya Yanga na Azam ambapo 'Wanajangwani' walionyesha soka la kitabuni na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Abedi Pele yupo nchini kwa ziara ya kuhamasisha maendeleo ya soka la vijana, mradi unaosimamiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA. mtoto mwingine wa Abedi Pele aitwaye Abdulrahim Ayew anacheza soka la kulipwa katika klabu ya Lierske inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.
No comments:
Post a Comment