Wednesday, November 21, 2012

MABAO MAWILI YAMFANYA LIONEL MESSI ASHIKE NAFASI YA PILI KWA WAFUNGAJI WA MUDA WOTE KATIKA LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA... AFIKISHA MABAO 56 NA KUMSHIKA VAN NISTEROOY... SASA AMFUNGIA KAZI RAUL ANAYEONGOZA KWA KUWA NA MABAO 71... !

MOSCOW, Urusi
Kama ilivyo kwa mvunja rekodi Roger Federer katika mchezo wa tenis, ndivyo straika wa Barcelona, Lionel Messi anavyofanya katika soka ambapo kila uchao amekuwa akivunja rekodi moja baada ya nyingine.

Mu-argentina huyo aliendelea na tabia yake hiyo ya kuvunja rekodi jana baada ya kufunga mabao mawili wakati klabu yake ikishinda 3-0 dhidi ya Spartak Moscow na kufuzu kwa hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Klagbu Bingwa Ulaya.

Magoli hayo mawili yaliongeza akaunti yake katika michuano hiyo ya UIaya kufikia 56, hivyo kumfanya awe wa pili katika orodha ya wafungaji, sawa na Mholanzi Ruud van Nistelrooy. Messi sasa anapitwa na Mhispania Raul tu ambaye yuko kileleni akiwa na mabao 71.

Messi pia amefikia rekodi ya Raul ya kufunga katika miji 19 tofauti katika Ligi ya Klabu Bingwa na kumpita straika huyo wa zamani wa Real Madrid kwa kufunga magoli mawili au zaidi katika mechi 14 za michuano hiyo.

Messi pia amebakiza mabao matano tu kufikia rekodi ya Gerd Mueller ya kufunga magoli 85 katika mwaka mmoja wa kalenda, ambayo aliiweka mwaka 1972.

Baada ya mechi kumalizika, mara moja Messi alipuuza magoli anayofunga kila uchao, lakini wachezaji wenzake hawakusita kumminia sifa.

"Leo anavunja rekodi zote, ni mkali, anatisha; ni furaha kubwa kuwa naye kikosini," Pedro aliiambia tovuti ya Barcelona (www.fcbarcelona.com).

Messi amekuwa mfungaji bora katika Klabu Bingwa Ulaya kwa miaka misimu minne mfululizo na msimu uliopita alifunga magoli 14 ambayo ni mengi kuliko yote katika msimu mmoja wa michuano hiyo.

"Kila mmoja anazungumza kuhusu Leo, magoli na rekodi lakini zaidi ni uelewa wake (katika mchezo) na mbinu, namna anavyozuia, kushambulia na kuisaidia timu katika kila eneo," kocha Tito Vilanova aliwaambia waandishi wa habari.


Katika mechi nyingine za jana, Man U waliowapumzisha nyota wao kibao baada ya kujihakikishia nafasi ya kwanza katika kundi lao walipata kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Galatasaray, Chelsea wakalambwa 3-0 na Juventus, Bayern na Valencia wakatoka sare ya 1-1 na Shakhtar Donetsk wakaifunga Nordsjaelland 5-2.

No comments:

Post a Comment