Sunday, November 4, 2012

KAVUMBAGU, KIIZA WAIPAISHA YANGA KWA KUFUNGA MABAO YALIYOWAPA USHINDI 2-0 DHIDI YA AZAM.... SIMBA KUMBE ILIKUWA IKIONGOZA KWA BAISKELI YA 'BARAFU'... YACHAPWA 2-0 NA MTIBWA SUGAR KWA MABAO MAKALI YA SAID MKOPI NA HUSSEIN JAVU... KASEJA AMWAGA CHOZI, ATAKA KUTWANGANA MANGUMI NA EMMANUEL OKWI... WANAJANGWANI SASA WAKWEA RASMI KILELENI MWA MSIMAMO WA LIGI WAKIWAACHA SIMBA KWA POINTI TATU..!

Dogo kama hunijui basi mie nd'o Fabregas wa Rwanda... Haruna Niyonzima 'Fabregas' wa Yanga (kulia) akimiliki mpira dhidi ya Salum Aboubakar 'Sure Boy' wa Azam wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.



Mabao kutoka kwa straika wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbagu na straika wa Uganda, Hamis Kiiza yaliipandisha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi 'mtamu' wa mabao 2-0 dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku mahasimu wao wa jadi, Simba wakipata kipigo cha ugenini cha 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro leo.

Kama ilivyokuwa kwa Yanga, Mtibwa walifunga mabao yao pia katika kila kipindi kupitia kwa mastraika wao nyota, Said Mkopi na Hussein Javu ambaye aliwahi pia kuiliza Yanga kwa kupiga 'hat-trick' wakati 'Wanajangwani' walipolala3-0 katika mechi yao ya raundi za mwanzo wa msimu.

Katika mechi ya Taifa, Yanga walionyesha soka safi kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho, wakigongeana pasi za kuvutia na kutawala mno katika eneo la katikati ya dimba lililokuwa chini ya himaya ya kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas'.

Kavumbagu ambaye sasa anaongoza katika orodha ya wanaowania kiatu cha dhahabu baada ya kufikisha magoli saba, aliifungia Yanga bao la utangulizi katika dakika ya tisa, aki
malizia gonga safi baina ya Niyonzima, Simon Msuva na Mbuyu Twite na Kiiza alifunga goli la pili ambacho Azam walipotea kabisa na kutumia muda mwingi 'kuusaka mpira kwa tochi' kutokana na 'gonga' za kusisimua zaidi za Yanga; zikiwamo zilizozaa bao la Kiiza ambalo pia lilitokana na "one-two' za Niyonzima, Kiiza mwenyewe na Chuji kabla mfungaji kukwamisha mpira wavuni.

Matokeo ya mechi za leo yameifanya Yanga ikwee rasmi kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Bara
kwa kufikisha pointi 26 baada ya mechi 12 huku Simba ikiangukia katika nafasi ya pili kwa kubaki na pointi zake 23. Azam inabaki kuwa ya tatu ikiwa na pointi 21, lakini ina mechi moja mkononi na wanaweza kuwashusha Simba hadi nafasi ya tatu kama watashinda mechi yao hiyo.

Kipigo cha leo kwa Simba inayoonekana kama ilitangulia na "baiskeli ya barafu" ni muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha kwa timu hiyo kila inapocheza ugenini kwani licha ya kuongoza kwa muda mrefu kutokana na ushindi mfululizo wa mechi zao nyingi za nyumbani; mabingwa hao watetezi walishashikiliwa kwa sare pia katika mechi dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT jijini Tanga, sare dhidi ya Kagera Sugar waliyocheza nayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na pia wakasimamishwa ugenini kwa sare isiyotarajiwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro dhidi ya 'maafande' wa Polisi Moro ambao hadi sasa ndiyo wanaoburuta mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo.



KASEJA AMWAGA CHOZI
Katika tukio jingine lisilokuwa la kawaida, kipa na nahodha wa Simba, Juma Kaseja alijikuta akimwaga chozi baada ya timu yake kulala katika mechi hiyo.

Kipa huyo pia nusra atwangane makonde na straika wao nyota wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi baada ya mechi kumalizika ambapo kwanza walionekana wakishutumiana kabla ya kutaka kuzichapa kavukavu. 

Hata hivyo, wachezaji hao nyota wa Simba walitenganishwa na kocha wao wa makipa, James Kisaka ambaye aliwahi kabla hawajarushiana makonde. 

Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic alisema amekubaliana na matokeo kwani ndio soka lilivyo hata hivyo hakuacha kuwatupia lawama waamuzi akisema wanachangia kushusha morari ya wachezaji. Judith Gamba kutoka Arusha ndiye aliyekuwa refa wa mechi hiyo.
 

Mecky Mexime, kocha wa Mtibwa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, alisema amefurahishwa na ushindi huo na kwamba pointi za jana zimewasaidia kwani walikuwa katika hali mbaya ingawa ligi bado ni ngumu.
 

Mwanasoka bora wa Afrika wa zamani, Abedi Pele, ambaye amekuja nchini katika programu maalum ya kuendeleza michezo ya FIFA, alitambulishwa uwanjani kabla ya mechi ya Yanga na Azam kuanza.


Kocha wa Azam, Hall alikiri kwamba walizidiwa kwa kila kitu katika mechi hiyo.
 

"Yanga wamecheza vizuri, walituzidi karibu katika kila idara, hatukujilinda vizuri, eneo la katikati palikuwa ovyo na safu yetu ya ushambuliaji haikucheza vizuri, kwa kifupi tumecheza ovyo. Cha muhimu ni kujipanga kwa ajili ya mechi zetu zilizobaki," alisema kocha huyo Muingereza.
 

Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na akaelezea furaha yake kwa mahasimu wao Simba kupoteza mechi yao ya kwanza.
 

"Timu imecheza vizuri licha ya makosa kadhaa katika dakika 20 za kwanza. Baada ya hapotulicheza vizuri kwa uelewano. Tumepata taarifa kuwa Simbawamepoteza mechi yao. Hiyo ni nzuri kwa sababu sasa tunaongoza ligi. Mwisho wa mechi hii ni mwanzo mzuri wa maandalizi ya mechi ijayo," alisema Brandts.

Katika mechi ya utangulizi, Yanga B iliifunga Azam B kwa mabao 2-0, ushindi uliomkosha aliyekuwa makamu mwenyekiti wa kllabu hiyo, Davis Mosha ambaye aliwazawadia yosso hao Sh. milioni 1 akishirikiana na wajumbe wa klabu hiyo, Bin Kleb na Mussa Katabaro.
 

Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa:
 

Azam:
Mwadini Ali, Erasto Nyoni/ Sahim Nuhu (dk.59), Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris, Said Morad, Bolou Michael, Salum Abubakar 'Sure Boy', Jabir Aziz Stima, John Bocco 'Adebayor', Kipre Tchetche na Mcha Khamis/ Abdi Kassim 'Babi' (dk. 62).
 

Yanga: 
Ali Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank domayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima.

Vikosi kwenye Uwanja wa Jamhuri vilikuwa: 


Polisi Moro: 

Hussein Shariff, Hassan Kessy, Issa Rashid, Rajab Zahir, Salum Sued, Shaban Nditi, Jamal Mnyate/ Ally Mohammed (dk. 48), Babu Ally, Mohammed Mkopi, Shabani Kisiga na Vincent Barnabas/ Said Mkopi (dk.90).  

Simba: 

Juma Kaseja, Shomary Kapombe, Amir Maftah, Komalmbil Keita, Pascal Ochieng, Jonas Mkude/ Ramadhani Chombo 'Redondo' (dk.68), Daniel Akuffor, Amri Kiemba, Felix Sunzu, Mwinyi Kazimoto na Emmanuel Okwi.

No comments:

Post a Comment