Wednesday, November 7, 2012

KASEJA NA WACHEZAJI WENGINE NANE SIMBA WAJAZANA KIKOSI KIPYA TAIFA STARS.... SAID BAHANUNZI, HARUNA MOSHI BOBAN, STEPHANO MWASIKA, TEGETE WATOSWA... NI KATIKA KIKOSI KILICHOTANGAZWA LEO NA KOCHA POULSEN KUJIANDAA MECHI DHIDI YA HARAMBEE STARS...!

Juma Kaseja
Nahodha wa Simba, kipa Juma Kaseja ameongoza orodha ya wachezaji tisa wa Simba waliojumuishwa katika kikosi kipya cha timu ya taifa, Taifa Stars kitakachocheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Kenya 'Harambee Stars' itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Katika orodha hiyo, kocha Kim Poulsen amewatosa pia nyota kadhaa waliokuwa wakiunda kikosi kilichopita cha Stars ambao ni pamoja na Haruna Moshi 'Boban' wa Simba na nyota wa Yanga, Jerry Tegete, Stephano Mwasika na Said Bahanunzi.

Poulsen amesema kuwa ameendelea kumteua Kaseja na kujumuisha wachezaji wengine katika kikosi chake kutokana na kiwango cha juu walichoonyesha wakati wakizichezea klabu zao.

Mbali na Kaseja ambaye uteuzi wake unaweza kuwashangaza baadhi ya mashabiki wa klabu yake wanaodai kwamba kiwango cha kipa huyo kimeporomoka na ndiyo maana klabu yao inapata matokeo mabaya katika siku za karibuni ikiwa ni pamoja na kipigo cha 2-0 walichopata kutoka kwa Mtibwa, wachezaji wengine wa Wanamsimbazi ni Nassoro Masoud “Cholo”, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Edward Christopher, Ramadhani Singano na Mrisho Ngassa.

Kikosi kamili cha wachezaji hao 22 waliotangazwa na Poulsen akiwa jijini Mwanza leo ni:
Makipa: Kaseja (Simba) na Deogratias Munishi (Azam)

Mabeki: Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris na Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa), Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe na Amir Maftah (Simba).

Viungo: Salum Abubakar “Sure Boy” (Azam), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano na Mrisho Ngassa (Simba), Athuman Iddi ‘Chuji” na Frank Domayo (Yanga) na Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar).

Washambuliaji: John Bocco (Azam), Simon Msuva (Yanga), Christopher Edward (Simba) na Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe)

1 comment: