Wednesday, November 7, 2012

AZAM YAPAA NAFASI YA PILI, SIMBA YAANGUKIA NAFASI YA TATU

Kiungo wa Azam, Kipre Bolou (wa pili kushoto) akimiliki mpira huku akichungwa na wachezaji wa JKT Oljoro wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam leo.
Kiungo wa Azam, Salum Aboubakar 'Sure Boy" (wa pili kulia) akimiliki mpira huku akichungwa na wachezaji wa JKT Oljoro wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam leo.

AZAM imeiengua Simba katika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kushinda goli 1-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam leo.


Ushindi huo unamaamsha kwamba kwamba Azam sasa imefikisha pointi 24, mbili nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 26, na moja juu ya watetezi Simba wenye pointi 23.


Coastal Union nayo imeutumia vyema uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani, Tanga baada ya kushinda 1-0 dhidi ya timu inayoshika mkia ya Polisi Morogoro na kufikisha pointi 22, moja tu nyuma ya Simba.

Nayo Mtibwa imeshinda 1-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye uwanja wa nyumbani wa Manungu, Turiani katika mechi nyingine ya ligi iliyowashuhudia wenyeji wakimaliza wakiwa tisa uwanjani baada ya nyota wao wawili Vincent Barbanas na Salum Machaku kutolewa kwa kadi nyekundu na refa Ibrahim Kidiwa wa Tanga kutokana na kutoa lugha chafu.

Mtibwa imebaki katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 19, moja nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 20 katika nafasi ya tano.

Matokeo hayo yanafanya mchuano kileleni mwa msimamo kuwa mkubwa na wa kiushindani zaidi huku timu zikiachana kwa pointi chache -- Yanga (pointi 26), Azam (24), Simba (23), Coastal (22), Kagera (20) na Mtibwa (19) baada ya timu zote kucheza mechi 12 kila moja.   

Daniel Lihanga aliifungia Coastal goli lao la ushindi katika dakika ya 3 na kuifanya timu hiyo ya Tanga ipande hadi nafasi ya nne ikiwa na pointi 22, moja tu nyuma ya Simba yenye pointi 23.


Issa Rashid alisherehekea kuitwa na kocha Kim Poulsen kwenye kikosi cha timu ya Taifa Stars kilichotajwa leo kwa kufunga goli lililoipa ushindi timu yake ya Mtibwa dhidi ya JKT Ruvu kwa juhudi binafsi akikimbia na mpira kutokea kwenye nusu yake ya uwanja hadi goli katika dakika ya 26.


Kwenye Uwanja wa Chamazi, Kipre Tchetche alifunga goli lake la saba msimu huu na kumfikia kinara wa mabao wa ligi Didier Kavumbagu wa Yanga katika dakika ya nne kwa njia ya penalti iliyotolewa na refa Livingstone Lwiza kutoka Kagera baada ya Yasin Juma kuunawa mpira ndani ya boksi, lakini wenyeji Azam walimaliza wakiwa 10 baada ya Himid Mao kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 88 kutokana na kumcheza rafu mchezaji wa Oljoro.


Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo unamalizika wikiendi hii kwa timu zote 14 kushuka uwanjani ambapo miongoni mwao, vinara Yanga watakuwa wageni wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Azam watawavaa Mgambo Shootings, Simba itawaalika Toto Africans.



DIDA, MORAD, ERASTO NYONI WASIMAMISHWA

Katika hatua nyingine, klabu ya Azam leo imewasimamisha nyota wake watatu wa kikosi cha kwanza kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu.

Kocha aliyerejea Azam, Muingereza Stewart Hall, amewasimamisha beki Said Morad, kipa Deogratius Munishi 'Dida' na kiungo Erasto Nyoni kwa muda wa wiki moja kwa utovu wa nidhamu.


Nyota hao hawakuwamo katika kikosi kilichocheza leo.

Hata hivyo, afisa habari wa Azam, Jaffer Idd alipoulizwa alisema jambo hilo si la kweli.
 

No comments:

Post a Comment