Saturday, November 3, 2012

JOSE MOURINHO: REAL MADRID ITAENDELEA KUWA MATAWI YA JUU HATA KAMA MIMI NA CRISTIANO RONALDO TUTAHAMA LEO KWENDA PSG YA UFARANSA..!

Gooooohh...! Cristiano Ronaldo akishangilia baada ya kufunga goli dhidi ya Barcelona.
MADRID, Hispania
Kocha wa Real Madrid,  Jose Mourinho amesema kuwa hatababaishwa ikiwa Cristiano Ronaldo ataihama klabu yake na kutimkia kwenye klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) inayoongoza katika Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa.

Ripoti za jana Ijumaa zilidai kwamba vigogo hao wa Ligue 1 wanaosifika kwa kumwaga fedha walikuwa tayari kutumja ofa nono ya kumtwaa straika huyo wa kimataifa wa Ureno kabla PSG hawajakanusha uvumi huo.

Mourinho amesema kuwa hakuna mchezaji aliye juu kuliko klabu na kwamba anaweza kuliona hilo sasa ambapo timu yake ya Real imekuwa ikifanya vizuri pia licha ya kuwakosa nyota wake kadhaa wa kikosi chao cha sasa.

"Naweza kuifikiria Real Madrid isiyokuwa na yeyote kati yetu," amewaambia waandishi wa habari.

"Kama Real Madrid inamilikiwa na mchezaji yeyote au kocha yeyote, litakuwa jambo baya na haingekuwa klabu yenye hadhi ya juu kama sasa. Real Madrid ni matokeo ya jumuiko la la mengi."

Real Madrid imeanza kwa kusuasua katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania msimu huu, ikishikilia nafasi ya nne na kuachwa kwa pointi nane na vinara ambao ni mahasimu wao wa jadi, Barcelona.

Wakati huohuo, Mourinho amesema hafurahishwi na dakika chache za kucheza anazopewa kiungo Jose Rodriguez katika kikosi cha Castilla – timu ya wachezaji wa akiba wa Real Madrid – na kocha wao wa vijana, Alberto Toril.

Yosso huyo mwenye miaka 17 amecheza mara sita msimu huu klabla ya kuitwa na Mourinho kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza cha Real wakatio wa mechi waliyoshinda 4-1 dhidi ya CD Alcoyano katika kuwania Kombe la Mfalme Jumatano.

"Jose Rodriguez, ambaye mnampenda sana, hapewi mechi kuichezea Castilla, wakati wengine wanapata licha ya kuwa na miaka 24. Kwakweli inahuzunisha," Mourinho amesema kabla ya mechi ya klabu yake dhidi ya Real Zaragoza inayochezwa leo (Jumamosi Novemba 3, 2012) kuanzia saa 4:00 usiku.

"Nina mamlaka yangu na Toril ana mamlaka yake. Nafanya kile ninachotaka katika kikosi cha wakubwa na yeye anafanya atakavyo katika kikosi cha cha pili. Ninaushauri, na ushauri wangu hautabadilisha kitu."

Mourinho amesema vilevile kuwa timu yake inahitaji kujifunza namna ya kushinda huku ikicheza bila ya kuvutia kama inataka iendelee kubaki katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu.

"Siri ya kushinda mechi? Ni kucheza vizuri," amesema.

"Timu nyingine zinashinda hata pale zinapocheza vibaya, lakini hilo haliko kwa Real Madrid."

No comments:

Post a Comment