Friday, November 16, 2012

FIFA YATANGAZA WANAOWANIA "TUZO YA GOLI BORA LA MWAKA 2012"... YAMO MAGOLI YA LIONEL MESSI, RADAMEL FALCAO NA NEYMAR... YA CRISTIANO RONALDO YATUPWA... AFRIKA YAMO MABAO YA MGHANA AGYEMANG BADU NA MOUSSA SOW... MASHABIKI KUCHAGUA HADI NOVEMBA 29

Lionel Messi
Radamel Falcao

Neymar
Agyemang Badu
Moussa Sow
Hatem Ben Arfa


ZURICH, Uswisi
Lionel Messi, Radamel Falcao na mshindi wa mwaka jana, Neymar ni miongoni mwa nyota waliochaguliwa na Shiriklisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuwania Tuzo ya Goli Bora la Mwaka maarufu kama Tuzo ya Puskás huku straika Cristiano Ronaldo aliyewahi kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza ilipoanzishwa miaka mitatu iliyopita akiambulia patupu baada ya kukosekana katika orodha hiyo.

Messi ambaye pia anawania Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa FIFA kwa mara ya nne mfululizo, ameingia katika kinyang'anyiro hicho kutokana na goli 'kali' aliloifungia timu yake ya taifa ya Argentina dhidi ya Brazil, na Mcolombia Falcao ameingia katika orodha kutokana na bao lake la kusisimua la shuti la 'tiktaka' aliloifungia klabu yake ya Atlético de Madrid katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya timu ya América de Cali ya nyumbani kwao Colombia.

Jopo la wataalam na wajumbe wa Kamati ya Soka ya FIFA wamechagua magoli 10 kuwania tuzo ya Puskas inayotolewa kwa mara ya nne. Katika miaka mitatu iliyopita, tuzo hiyo imewahi kubebwa na Cristiano Ronaldo, Mturuki Hamit Altintop na Mbrazil Neymar.

Mashabiki wanapewa nafasi ya kurejea video za mabao hayo kupitia tovuti (http:////www.fifa.com/ballondor/puskasaward/index.html) na kupiga kupiga kura hadi kufikia Novemba 29, 2012 kabla ya kuchujwa na kutangazwa magoli matatu ya mwisho yatakayotinga fainali kuwania tuzo hiyo. 

Tovuti hiyo pia itatoa nafasi kwa mashabiki kupiga kura ya kuchagua goli bora hadi kufikia Januari 7, 2013 -- siku ambayo pia itatolewa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka (FIFA Ballon d'Or).

Messi alifunga goli lake 'kali' mwezi Juni, wakati alipopiga shuti 'tamu' baada ya kuwatoka mabeki kama kawaida yake kutokea kona ya kulia mwa uwanja , wakati Falcao alifunga goli zuri la shuti la 'baiskeli' baada ya kuunganisha kona iliyochongwa na Diego katika mechi yao ya kirafiki mwezi Mei.

Wengine ni Neymar anayefukuzia tuzo hiyo kwa mara ya pili baada ya kufunga goli 'kali' kutokana na juhudi binafsi za kukimbia na mpira kutoka katikati ya uwanja, na washirki wengine wakiwa ni Agyemang Badu (Ghana), Hatem Ben Arfa (Newcastle), Eric Hassli (Vancouver Whitecaps), Olivia Jiménez (Mexico), Gastón Mealla (Nacional Potosí) na wachezaji wawili wa klabu ya Fenerbahçe ya Uturuki ambao ni Moussa Sow na Miroslav Stoch.

No comments:

Post a Comment