Friday, November 16, 2012

ARSENE WENGER AKIRI KUTOMSAJILI ZLATAN IBRAHIMOVIC ALIYEKUWA AMETUA ARSENAL AKIWA YOSSO WA MIAKA 16... ALIWAHI PIA KUMKATAA DIDIER DROGBA KWA ADA POA YA PAUNDI 500,000... YAYA TOURE PIA ALIMFUNGIA VIOO ALIPOVUTWA NA KAKA YAKE KOLO TOURE ILI ASAJILIWE "BURE" NA ARSENAL MSIMU WA 2003/2004Zlatan Ibrahimovic

Didier Drogba

Yaya Toure
LONDON, England
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri kwamba walishindwa kirahisi kumsajili straika nyota wa klabu ya PSG ya Ufaransa na timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic wakati alipokuwa yosso wa miaka 16 lakini akaeleza sababu za kumkosa.

Ibrahimovic alikuwa amenasa katika rada za Arsenal tangu alipokuwa "serengeti boy" mwenye miaka 16 tu mwanzoni mwa soka lake.

Lakini baada ya 'kuiadhiri' England juzi kwa kuipiga mabao yote manne na kufunga jingine kali la "baiskeli" litakalobaki kwenye kumbukumbu kwa muda mrefu wakati Sweden ikishinda 4-2 dhidi ya England, Wenger hatimaye ameamua kueleza sababu za klabu yake kutomsajili nyota huyo.

"Alikuja hapa kutembelea uwanja wetu wa mazoezi," kocha huyo Mfaransa aliiambia arsenal.com.

"Hakutaka kufanya nasi majaribio kwa sababu wakati huo alikuwa ndiyo kwanza ana miaka 16. Alirudi kwao na tukakubaliana kuwa tutamuangalia tena.

"Nilitaka kumuona mazoezini, lakini hilo halikumzuia kusonga mbele kwa mafanikio. Mwishowe alichagua kwenda Ajax Amsterdam. Haya yanatokea. Wala si yeye peke yake wa namna hii.

"Kujiamini anakoonyesha… kama hana kiwango mnaweza kusema (kwamba) hamkubaliani naye, lakini kama anaonyesha kiwango, mnaona wazi (kuwa) kujiamini kwake kunaelezeka. Katika kazi yake, amethibitisha ni kwanini hujidai kutokana na kipaji chake."

Mbali na Ibrahimovic, Wenger pia aliwahi kuwakataa yosso wengine kadhaa ambao baadaye walikuwa nyota wa soka wa kimataifa, baadhi yao wakiwa ni Didier Drogba ambaye Wenger aliwahi kukataa kumsajili wakati alipokuwa yosso kwa ada poa ya paundi za England 500,000 (Sh. bilioni 1.2). Drogba akatisha sana baadaye na alipojiunga na Chelsea, akaifunga Arsenal ya Wenger magoli 13 katika mechi 14 alizokutana nayo, huku mechi moja tu kati ya hizo ambayo Arsenal ilishinda dhidi ya Chelsea iliyokuwa na Drogba.

Wenger pia aliwahi kumkataa kiungo nyota wa Manchester City, Yaya Toure ambaye alipelekwa Arsenal na kaka yake Kolo Toure (aliyekuwa Arsenal) ili akifuzu asajiliwe 'bure' mwaka 2003. Yaya aliishia kutoswa baada ya kutofanya vizuri katika majaribio wakati alipochezeshwa kama mshambuliaji wa kati.

Yaya akaondoka kwa unyonge na kutimkia katika klabu za Beveren ya Ubelgiji aliyokuwa nayo hapo kabla, Metalurh Donetsk ya Ukraine, Olympiacos ya Ugiriki, Monaco ya Ufaransa, Barcelona ya Hispania na sasa ni miongoni mwa nyota wa mabingwa wa Ligi Kuu ya England, klabu ya Manchester City na pia timu ya taifa ya Ivory Coast.

1 comment: