Wednesday, November 21, 2012

DI MATTEO ATIMULIWA UKOCHA CHELSEA

Roberto Di Matteo

KOCHA Roberto Di Matteo ameachia ngazi baada ya Chelsea kukumbana na kipigo cha 3-0 dhidi ya Juventus katika mechi yao ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya jana usiku, klabu hiyo imetangaza leo.

Di Matteo alitwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na kombe la FA msimu uliopita akiwa kocha wa muda na akapewa mkataba wa miaka miwili Juni mwaka huu.

Lakini baada ya kipigo cha 3-0 kutoka kwa Juventus, ambacho kimewaacha The Blues wakiwa hatarini kuaga michuano hiyo ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ameondoka Stamford Bridge.

"Klabu itatoa taarifa muda mfupi kuhusu kocha mkuu," taarifa ilisema.

Baada ya kuanza msimu kwa kishindo, The Blues wameshinda mechi mbili tu kati ya nane zilizopita.

Wameangukia katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu ya England, pointi nne nyuma ya vinara Manchester City.

Taarifa iliendelea: "Kiwango cha timu katika siku za karibuni si kizuri na mmiliki na bodi imeona kwamba ni muafaka kufanya mabadiliko ili kuiwezesha klabu kuendelea kusonga mbele katika upande sahihi wakati tunaingia katika kipindi muhimu cha msimu.

"Klabu inakabiliwa na kazi ngumu ya kuwania kufuzu kwa hatua ya mtoano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya pamoja na kupambana katika ushindani mgumu kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England huku tukichuana pia katika kuwania makombe mengine matatu.

"Lengo letu ni kubaki katika mwendo mzuri iwezekanavyo na kupambana kwa nguvu katika michuano yote."

No comments:

Post a Comment