Saturday, November 24, 2012

BRAZIL WAMTIMUA KOCHA WAO MANO MENEZES... WAHOFIA KUWA ATASHINDWA KUWAFANYA KINA NEYMAR WATISHE KATIKA FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA 2014

Mano Menezes
RIO DE JANEIRO, Brazil
Brazil wamemtimua kocha wao mkuu, Mano Menezes wakati wakitafuta "mbinu mpya" kuelekea fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kwenye ardhi yao mwaka 2014.

Menezes, 50, alirithi nafasi iliyoachwa na Dunga baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia 2010, akiiongoza Brazil kufika robo fainali ya Copa America mwaka 2011.

Kipigo kutoka kwa Paraguay, pamoja na "kuchemsha" kwa Brazil kutekeleza nia yao ya kutwaa medali ya dhahabu kwenye michuano ya Olimpiki jijini London 2012, ndivyo vilivyochangia kuondoshwa klwa kocha huyo.

Uamuzi huo umekuja siku mbili tu baada ya Brazil kutwaa taji la Amerika Kusini la 'Superclasico' dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Argentina.

Brazil walifungwa 2-1 katika mechi yao ya marudiano mjini Buenos Aires, lakini wakaibuka kidedea kwa mikwaju ya penati katika mechi iliyohusisha nyota wanaocheza ligi kuu za nyumbani tu katika nchi hizo mbili, akiwamo Neymar wa klabu ya Santos ya Brazil.

Mkurugenzi wa Shirikisho la Soka la Brazil, Andres Sanchez alisema kuwa Jose Maria Marin amefanya mabadiliko kwa sababu "anataka mbinu mpya na mipango mipya" kuelekea fainali za Kombe la Dunia.

No comments:

Post a Comment