Monday, November 5, 2012

ABEDI PELE ATAKA WATANZANIA WACHEZE MATAIFA YA AFRIKA


NYOTA wa zamani wa Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa, Abedi Pele, amewaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kuwa "hakuna njia ya mkato katika kutafuta mafanikio" na kuwataka kufanya jitihada ili watimize ndoto, ikiwa ni pamoja na Serengeti Boys kuhakikisha inafuzu kucheza fainali za Afrika mwakani.

Pele, ambaye aliiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao dhidi ya AC Milan ya Italia, alisema hayo jana asubuhi wakati alipotembelea Kituo cha Ufundi cha Karume kushuhudia programu ya mazoezi ya vijana wadogo inayofanyika kila mwisho wa wiki kwenye Uwanja wa Karume ambako watoto wa kuanzia umri wa miaka sita hadi 17 hufundishwa mbinu za kusakata soka.

"Katika kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye ameletwa nchini na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) kuangalia shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

"Tunaona wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze kucheza kwa kiwango cha juu. Bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria huwezi kufanikiwa.

"Wale wenye vipaji vikubwa, lakini hawafanyi jitihada watabakia chini. Wale wasiojaliwa kuwa na vipaji, lakini wanafanya jitihada watakwenda mbele na kupata mafanikio," alisema nyota huyo wa Ghana ambaye alijijengea jina kwa kufunga mabao safi na muhimu kwa nchi yake na klabu ya Olympique Marseille wakati ikitamba katika soka barani Ulaya.

"Soka barani Afrika lina mazingira yanayofanana. Hakuna mtoto wa waziri anayecheza soka. Wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi wa benki ambaye anacheza soka. Soka linachezwa na watu wanaotoka kwenye familia ambazo hazina maisha mazuri na hivyo mna nafasi sawa na wengine wote. Mnachotakiwa kufanya ni kujituma, kudhamiria na kufanya jitihada ili mfungue mlango wa mafanikio."

Pele, ambaye jina lake halisi ni Abedi Ayew na ambaye watoto wake wanaichezea Marseille, pia aliwataka wachezaji wa timu ya taifa ya vijana walio na umri china ya miaka 17 kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Algeria mapema mwakani.

"Mkifuzu mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu," alisema gwiji huyo ambaye anaiwakilisha FIFA katika kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo.

"Nikiwaangalia naona mna uwezo wa kuwaondoa wapinzani wenu na nitafuatilia mechi yenu. Mkifuzu tutakuwa wote na nitawaunga mkono."

Pele, ambaye kwa sasa anamiliki shule ya mpira wa miguu ambayo imeshatwaa Kombe la FA mara moja, ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo wa FIFA kwa nchini za Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na mmoja wa viongozi wa Idara ya Mawasiano ya FIFA, Emmanuel, atakuwa nchini kwa siku tatu ambazo atazitumia kupata taarifa za shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo za soka la watoto (grassroots), soka la vijana, soka la wanawake na miradi mingine ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment