Wednesday, November 14, 2012

AGGREY MORRIS AWANYAMAZISHA KINA OLIECH TAIFA STARS IKIIZAMISHA HARAMBEE STARS

Beki wa kati wa Taifa Stars, Aggrey Morris(jezi Na.6) akipongezwa na wachezaji wenzake baada ya kufunga goli la ushindi dhidi ya Harambee Stars ya Kenya katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza leo.


BEKI wa kati, Aggrey Morris, alifunga goli pekee lililoamua mechi wakati Taifa Stars ilipopata ushindi wa 1-0 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya katika mechi yao ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo.

Baada ya kutumia wiki hii akikanusha uvumi kwamba alihusika katika tuhuma za rushwa zinazowakabili wachezaji kadhaa wa klabu yake ya Azam FC, Morris alipaa hewani zaidi ya mabeki wa Harambee Stars na kufunga goli hilo kwa kichwa kufuatia krosi ya beki mwenzake Amir Maftah. 


Kocha wa Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen, alionekana kufurahishwa na ushindi huo lakini anaamini kwamba wangeweza kupata ushindi mnono zaidi.

"Unapopata nafasi ya kumaliza mechi mapema ni vyema ukaitumia. Tulikuwa na nafasi ya kumaliza mechi mapema. Na tungeweza kushinda kwa magoli 2-0 ama 3-0. Nadhani tulistahili kushinda. Hatukuwa na muda wa kutosha wa kukaa kambini na hatukufanya mazoezi vizuri leo, lakini sasa tutakaa kambini na kwa timu hii changa tunayo nafasi ya kuwa na timu nzuri zaidi," alisema.


Harambee Stars iliwakosa nyota wake wawili wanaocheza Ulaya, Victor Wanyama wa Celtic ya Scotland na kaka yake McDonald Mariga, lakini walikuwa na mshambuliaji Denis Oliech wa Auxerre ya Ufaransa na wakali wengineo, ambao hata hivyo hawakuweza kuzigusa nyavu za kipa na nahodha, Juma Kaseja.

Mbwana Samatta alikuwa tishio katika lango la wageni ambalo liliandamwa kwa ushirikiano wake na nyota mwenzake wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu na winga 'teleza' Mrisho Ngassa.

Kaseja, ambaye amekuwa katika presha ya baadhi ya mashabiki wa klabu yake ya Simba wanaomtuhumu kushuka kiwango, alikuwa nguzo muhimu langoni leo akiokoa hatari kadhaa na mwisho wa mechi aliwashukuru mashabiki wa soka wa Mwanza kwa kujitokeza kuwapa sapoti ilisaidia ushindi huo.


Stars haitavunja kambi yake ya jijini Mwanza kwa ajili ya kujiandaa mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayoanza Novemba 24 mjini Kampala, Uganda. 

Hata hivyo, itampoteza mfungaji wa goli la ushindi la leo Morris, na beki Nasoro Said 'Chollo', ambao wataenda kujiunga na kambi ya timu ya taifa ya Zanzibar Heroes.

Vikosi vya leo vilikuwa; Taifa Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah/ Nasoro Said 'Chollo' (dk.67), Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa/ Shabani Nditi (dk.79), Salum Aboubakar 'Sure Boy'/ Amri Kiemba (dk.65), Thomas Ulimwengu/ Issa Rashid "Baba Ubaya" (dk.88), Mwinyi Kazimoto/ Simon Msuva (dk. 65) na Mbwana Samatta/ John Bocco (dk.85).

Harambee Stars: Fredrick Onyango, Brian Mandela, Augene Asike, James Situma/ Christopher Wekesa (dk. 45), Edwin Wafula, Jerry Santo/ Anthony Akumu (dk. 45), Peter Opiyo/ Charles Okwemba (dk. 67), Patrick Obuya, Patrick Osaika/ Mulinge Ndeto (dk. 73), Denis Oliech, Wesley Kemboi/ Timbe Ayub (dk.45).

No comments:

Post a Comment