Wednesday, October 24, 2012

YANGA YAIWASHIA SIMBA INDIKETA, AZAM YASHIKWA, COASTAL YAPIGA MTU... MCHUANO KILELENI MWA MSIMAMO SI WA KITOTO

Mchezaji wa Yanga, Simon Msuva (kushoto) akiruka daruga la John Bosco wa Polisi Moro wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Simon Msuva (kushoto) wa Yanga akishangilia baada ya kuifungia timu yake goli la kuongoza dhidi ya kipa wa Polisi Morogoro, Manji Kulwa (aliyelala chini) wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

MAGOLI kutoka kwa Simon Msuva, Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza, yameipa Yanga ushindi wa kujiamini wa magoli 3-0 dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni na kujiimarisha katika nafasi ya tatu, lakini Azam imeshindwa kuwaengua vinara Simba kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kung'ang'aniwa kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Chamazi dhidi ya Ruvu Shootings ya mkoani Pwani.    

Coastal Union ya Tanga nayo imepata ushindi wa 1-0 dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mkwakwani kupitia goli pekee la mshambuliaji Nsa Job,  na kufanya kinyang'anyiro kileleni mwa msimamo kiwe cha kuvutia mno.


Vinara Simba wana pointi 19 na wanafuatiwa kwa karibu na Azam yenye pointi 18, Yanga (pointi 17) na Coastal Union yenye pointi 16 katika vita ambayo haijawahi kutokea katika miaka ya karibuni.

Vita ya kileleni inatarajiwa kunoga zaidi Jumamosi katika mpambano wa timu mbili za juu wakati Simba itakapoikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Taifa, huku Yanga wakiwa wageni wa JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha. Coastal Union watakuwa wageni wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Chamazi Jumapili.

Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zimetoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro. Goli la wenyeji Mtibwa limefungwa na Jamal Mnyate wakati la Kagera Sugar limetupiwa na Mnigeria Wilfred Emmeh.

Yosso Simon Msuva aliifungia Yanga goli la kuongoza mapema katika dakika ya 5 akitumia makosa ya mabeki wa Polisi, Salimin Kisi na Hamisi Mamiwa, waliodhani ameotea.

Mshambuliaji Didier Kavumbagu aliiongezea Yanga goli la pili dakika moja baadaye baada ya kuwazidi kasi mabeki wa timu ya Polisi, ambayo kufikia sasa imeruhusu magoli 8 na kubaki timu pekee ambayo haijafunga goli hata moja tangu ilipopanda daraja msimu huu. Polisi iliyocheza mechi 7 imepoteza tano na imetoka sare 2 -- zote bila ya magoli.


Kiiza aliyeingia katika dakika ya 54 kuchukua nafasi ya Jerry Tegete, alihitaji dakika tatu tu uwanjani kuipatia Yanga goli la tatu katika dakika ya 57 akiunganisha pasi ya jirani na lango kutoka kwa David Luhende.


Haruna Niyonzima, angeweza kuipa Yanga ushindi mnono zaidi katika dakika ya 38 lakini penalti aliyopiga iligonga nguzo na kuokolewa na mabeki wakati kipa
Kondo Salum akiwa tayari ameruka upande mwingine. Penalti hiyo ilitolewa na refa Alex Mahagi kutoka Mwanza baada ya Msuva kuvutwa shati ndani ya boksi na beki wa Polisi.

Polisi walimpoteza kipa wao, Manji Kulwa mapema katika dakika ya 19 baada ya kuumia wakati alipookoa kishujaa shuti la jirani ya lango kutoka kwa Jerry Tegete aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, na nafasi yake ikachukuliwa na Kondo Salum.


Azam walihitaji ushindi ili kuiengua Simba kileleni mwa msimamo lakini walishangazwa na goli mapema katika dakika ya kwanza kutoka kwa Seif Rashid.


Winga wa Ivory Coast, Kipre Tchetche aliwasawazishia Azam goli hilo katika dakika ya 29 kufuatia piga nikupige langoni mwa Shootings. Azam bado wana mechi moja mkononi.

Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; 

Yanga: 
Ali Mustapha 'Barthez', Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Haruna Niyonzima/ Nurdin Bakari (dk.54), Jerry Tegete/ Hamisi Kiiza (54), Didier Kavumbagu na David Luhende/ Nizar Khalfani (dk.77).

Polisi Moro: 

Manji Kulwa/ Kondo Salum (dk.19), Nahodha Bakari, John Bosco, Noel Msakwa, Salmin Kisi, Hamisi Mamiwa, Bantu Admin/ Paul John (dk.72), Paschal Maige, Mokili Rambo, Malimi Busungu na Nicholas Kabipe/ Keneth Masumbuko (dk.50)

Msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya mechi za leo:

                                  P    W  D   L    GF  GA GD Pts
1. Simba                     9    5    4    0    16   6    10    19
2. Azam                      8    5    3    0     9    3    7    18
3. Yanga                     9    5    2    2    17  10   7    17
4. Coastal Union         9    4    3    2    11  8     3    16
5. JKT Oljoro              8    2    5    2    7    8     -1   11
6. JKT Mgambo          8    3    2    3    6    4     2    10
7. Kagera Sugar         8    2    4    2    8    7     1     10
8. Prisons                   8    2    4    2    5    5     0    10
9. Ruvu Shootings      9    3    1    5   12  14    -2     10
10. Mtibwa Sugar        8    2    3    3    9    9     0     9
11. JKT Ruvu              8    2    2    4    7    13   -6     8
12. African Lyon          9    2    1    6    5    12   -7     7
13. Toto African          8    1    3    4    7    11   -4     6
14. Polisi Moro            7    0    2    5    0     8    -8     2

No comments:

Post a Comment