Kiungo wa Arsenal, Mikel Arteta akimchezea faulo mchezaji wa Schalke 04, Ibrahim Afellay (kulia) wakati wa mechi yao Kundi B la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mjini London Oktoba 24, 2012. Picha: REUTERS |
LONDON, Uingereza
BORUSSIA Dortmund ilipanda kileleni mwa Kundi D la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya ushindi iliostahili wa 2-1 dhidi ya mabingwa wa Hispania, Real Madrid.
Goli la kuongoza la Robert Lewandowski kwa timu hiyo ya Ujerumani lilisawazishwa haraka na Cristiano Ronaldo lakini beki Marcel Schmelzer aliwafungia Dortmund goli la ushindi.
Porto na Malaga waliboresha rekodi yao ya ushindi wa asilimia 100 katika michuano ya mwaka huu na kuongoza makundi yao.
Porto waliifunga Dynamo Kiev 3-2 katika Kundi A wakati Malaga walipata ushindi wa 1-0 nyumbani dhidi ya AC Milan katika Kundi C.
Ulikuwa ni ushindi mwingine wa kuvutia kwa Malaga, ambao walikosa penalti ya dakika ya 45 kabla ya kuwafunga mabingwa mara saba wa Ulaya.
Joaquin Sanchez alikuwa mkosaji, akigongesha 'besela' penalti yake baada ya Kevin Constant kumuangusha Jesus Gamez.
Lakini Sanchez alirekebisha makosa katikati ya kipindi cha pili wakati aliunganisha pasi ya Manuel Iturra kwa shuti lililomshinda kipa Marco Amelia kutokea katika upande mgumu wa pembeni.
Klabu hiyo ya Italia imebaki ya pili katika Kundi C, baada ya Zenit St Petersburg kuifunga Anderlecht 1-0 kupitia goli la Alexander Kerzhakov aliyefunga penalti iliyofuatia Milan Jovanovic kumchezea faulo Alexander Anyukov.
Porto waliongoza mara tatu dhidi ya Dynamo Kiev kwenye Uwanja wa Estadio do Dragao, huku goli la Jackson Martinez likiamua matokeo dakika 12 kabla ya mechi kumalizika.
Kabla ya hilo, Silvestre Varela aliuwahi mpira wa krosi ya Lucho Gonzalez na kuwapa mabingwa hao wa mwaka 2004 uongozi, ambao uliofutwa na goli la kichwa kutokea jirani na lango kutoka kwa Oleg Gusev.
Dhamira ya Porto ya kuwa na mwanzo bora zaidi kwa mara ya kwanza tangu mwaka msimu wa 1999-2000, ilirejea wakati Mcolombia Martinez alipoipokea pasi ya kupenyezewa ya James Rodriguez na kumzunguka Yevgen Khacheridy kabla ya kumfunga kipa Alexander Shovkovskiy.
Brown Ideye aliisawazishia Dynamo kwa shuti lililobadilishwa mwelekeo baada ya kumgonga beki na kumpita kipa Helton lakini Porto hawakunyimwa mwanzo mzuri wakati Martinez alipofunga goli lake la pili na kupata pointi 3.
Paris St Germain ni wa pili katika Kundi A, pointi tatu nyuma ya Porto, baada ya magoli kutoka kwa Zlatan Ibrahimovic - goli lake la 12 msimu huu kwa klabu na taifa lake - na Jeremy Menez kuwapa ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Dinamo Zagreb.
Mjini Dortmund, kikosi cha kocha Jurgen Klopp kilihakikisha Real Madrid wanaendeleza rekodi yao mbovu ya kwenye ardhi ya Ujerumani.
Klabu hiyo ya Hispania imekumbana na vipigo 17 katika mechi 24 walizocheza nchini Ujerumani, huku ushindi wao wa mwisho ukija miaka 12 iliyopita.
Walionekana kama vile wangeondoka na kitu katika mechi hiyo wakati Ronaldo alipoupitisha mpira juu ya kipa Roman Weidenfeller na kutinga wavuni na kusawazisha dakika mbili tu tangu Lewandowski alipowafungia wenyeji goli la kuongoza.
Lakini Borussia ndiyo iliyokuwa timu iliyocheza vizuri zaidi na juhudi zao zikazaa matunda wakati Schmelzer alipofunga kwa shuti la kutokea kwenye ukingo wa boksi katika dakika ya 64.
"Tunajisikia furaha sana. Ilikuwa ni jioni nzuri, na ni vigumu kuota kwamba jambo kama hili linaweza kutokea hata katika ndoto zako za kiwazimu," alisema kocha wa Dortmund, Jurgen Klopp.
Kocha wa Madrid, Jose Mourinho alisema: "Ilikuwa mechi ya ajabu. Hakuna timu iliyokuwa bora zaidi ya nyingine, lakini ilikuwa mechi ngumu.
"Walikuwa wamejipanga vizuri na walijilinda vyema. Dortmund walistahili ushindi, lakini tulikuwa na nafasi zetu za kushinda mechi hii."
Matumaini ya Manchester City ya kutinga hatua ya mtoano ilipata pigo jingine kufuatia kipigo cha 3-1 ugenini dhidi ya Ajax.
Samir Nasri aliifungia Man City goli la kuongoza tofauti na mwelekeo wa mechi mjini Amsterdam, lakini Siem de Jong aliisawazishia Ajax kwa shuti la chini kabla ya mapumziko na Niklas Moisander akafunga goli la kichwa lililowapa uongozi.
Christian Eriksen akafanya matokeo yawe 3-1 kwa shuti ambalo lilimgonga Gael Clichy na kubadili mwelekeo.
Man City watawakaribisha Ajax Novemba 6 na Real Madrid Novemba 21 kabla ya kumaliza na Borussia Dortmund Desemba 4.
Dortmund wanaongoza kundi wakiwa na pointi saba, moja juu ya Real na tatu juu ya Ajax. Timu mbili zitasonga mbele kwenda hatua ya 16-Bora.
Kipigo kimewaacha Man City mkiani mwa Kundi D wakiwa na pointi moja baada ya mechi tatu.
Kundi B lina vita ngumu sasa baada ya Arsenal kufungwa nyumbani dhidi ya Schalke na huku Olympiakos ikipata ushindi wa 'usiku' dhidi ya Montpellier.
Arsenal iliyowakosa nyota wake kama Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain, Gibbs, Abou Diaby, Jack Wilshere, Bacary Sagna, ilionekana kukosa makali na ikafungwa magoli mawili ndani ya dakika 15 za mwisho kutoka kwa Klaas Jan-Huntelaar na Ibrahim Afellay na kuwapa Wajerumani ushindi waliostahili wa 2-0 kwenye Uwanja wa Emirates. Kilikuwa ni kipigo cha kwanza nyumbani kwa Arsenal tangu mwaka 2003.
Goli la dakika za majeruhi la Kostas Mitroglou liliipa timu hiyo ya Ugiriki pointi zao za kwanza za michuano hiyo msimu huu baada ya Vasilis Torosidis kusawazisha goli la Gaetan Charbonnier kwa wenyeji.
Olympiakos sasa wako pointi tatu nyuma ya Arsenal, ambao wanawafuatia Schalke kwa pointi moja. Montpellier wako mkiani wakiwa na pointi moja.
No comments:
Post a Comment