Wednesday, October 24, 2012

LORD EYEZ KUBURUZWA KORTINI KWA WIZI… ADAIWA YEYE NA WENZAKE NI VINARA WA KUVUNJA VIOO NA MILANGO YA MAGARI YANAYOKUWA KWENYE PARKINGS JIJINI DAR ES SALAAM NA KUKOMBA VITU KAMA POWER WINDOW, LAPTOPS, SIMU, POCHI…!

Lord Eyez

MSANII wa muziki wa kizazi kipya wa kundi la Weusi, Issa Waziri a.k.a Lord Eyez ama Lord Easy (28) atafikishwa mahakamani siku yoyote kuanzia kesho pamoja na watuhumiwa wenzake wawili wanaokabiliwa na kosa la wizi wa vifaa vya magari na vitu vingine vinavyohifadhiwa kwenye magari kama laptops, redio na mabegi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema hatua ya kuwapeleka kina Lord Eyez imefikiwa baada ya watuhumiwa kukutwa na vielelezo kadhaa kuhusiana kosa wanalotuhumiwa nalo.

Kenyela alisema kuwa msanii huyo na watuhumiwa wenzake, Kurshide Hillary (22) na Joseph Martini (24), wote wakazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, walikuwa wakiiba katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam pamoja na mikoa ya jirani kwa kutumia magari ya kukodi, pikipiki na bajaji, kwa mbinu ya kuegesha katika magari mengi wanayolenga kuyafanyia uhalifu.

Aliendelea kusema kuwa walikuwa wakipaka kimiminika maalumu katika kioo cha gari kinachorahisisha kazi ya kupasua na kisha kufungua mlango wa gari na kuiba.

Awali Kamanda Kenyela alithibitisha kuwa jeshi lake linamshikilia msanii huyo ambaye toka wiki iliyopita taarifa zake zilisambaa baada ya kuhusika na wizi wa vifaa mbalimbali kwenye gari la msanii mwingine nyota wa bongofleva, Ommy Dimpoz.

Alisema kukamatwa kwa msanii huyo kulitokana na taarifa walizozipata kutoka kwa Kurshde mwenye asili ya Kiasia aliyekamatwa Jumatatu iliyopita katika maeneo ya Kinondoni na alipohojiwa kwa kina, ndipo alipowataja wenzake akiwamo Lord Eyez. 


Nyota huyo alipata umaarufu mkubwa akiwa na kundi la Nako2Nako Soldiers la Arusha lililotamba na 'ngoma' kama 'Hawatuwezi' na 'We Mchizi Wangu' na alikuwa mchumba wa mwanadada Ray C ambapo walipata kutangaza kwamba walikuwa mbioni kufunga ndoa kabla ya kutengana baadaye. 

No comments:

Post a Comment