Wednesday, October 31, 2012

YANGA YAIVUTA MKIA SIMBA KILELENI, YONDANI AREJEA UWANJANI KWA MARA YA KWANZA TANGU ALIPOUMIZWA NA BOBAN

Chezea mimi wewe?...... Mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu akishangilia baada ya kuifungia timu yake goli la pili wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo jioni. Yanga ilishinda 3-0.
Simon Msuva wa Yanga (kushoto) akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa Mgambo JKT wakati wa mechi yao ya ligi kuu ya Tanzania bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

YANGA iliyokuwa na mwanzo mbaya wa msimu, hatimaye imeifikia Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Mgambo JKT, huku Wekundu wa Msimbazi waking'ang'aniwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya timu ya mkiani ya Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jioni ya leo. 


Ushindi huo unamaanisha kwamba Yanga sasa imelingana pointi 23 na Simba kileleni baada ya mechi 11. Hata hivyo, Simba yenye wastani wa magoli 12, inaendelea kuongoza ligi kwa wastani wa goli moja zaidi ya Yanga yenye wastani wa magoli 11. Simba imefunga magoli 20 na kufungwa 8 wakati Yanga imefunga magoli 21 na kufungwa 10.

Yanga ilianza kuhesabu goli la kwanza katika dakika ya pili tu ya mchezo kupitia kwa beki wake wa kati Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyefunga kwa kichwa kufuatia mpira wa 'fri-kiki' uliopigwa na kiungo Haruna Niyonzima.


Mshambuliaji Didier Kavumbagu aliifungia Yanga goli la pili katika dakika ya 39 kufuatia krosi ya Hamis Kiiza na Jerry Tegete akakamilisha ushindi wa kujiamini wa timu yake wakati alipofunga goli la tatu katika dakika ya 79 kufuatia pasi ya Oscar Joshua.

Ulikuwa ni ushindi wa saba katika mechi 11 kwa Yanga na kuwasahaulisha mashabiki wao mwanzo mbaya wa msimu uliowafanya wamfukuze kocha Mbelgiji Tom Saintfiet aliyedumu nao kwa siku 80 tu huku akiwa ameshawapa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Yanga pia ilifurahia kurejea kwa beki wake wa kati, Kelvin Yondani, aliyecheza kwa mara ya kwanza tangu aliponusurika kuumia vibaya zaidi katika rafu mbaya ya "vunja mifupa" aliyochezewa na kiungo Haruna Moshi 'Boban' wa Simba katika mechi ya watani wa jadi Oktoba 3. Aliingia katika dakika ya 46 akichukua nafasi ya beki veterani wa kulia, Shadrack Nsajigwa.   

Mambo hayakuwa mazuri kwa mabingwa Simba ambao walitanguliwa kwa goli la dakika ya 33 kutoka kwa Mokili Lambo, aliyekuwa ameingia uwanjani dakika 5 tu zilizopita kuchukua nafasi ya John Bosco aliyepumzishwa katika dakika ya 28.

Simba walirejea kipindi cha pili wakiwa nyuma kwa goli 1-0 kabla ya kiungo wao aliye katika kiwango cha juu tangu kuanza kwa msimu huu Amri Kiemba kuwasazishia katika dakika ya 57 akimalizia kona iliyochongwa na Emmanuel Okwi.


Ilikuwa ni sare ya 5 katika mechi 7 zilizopita za Simba baada ya kushinda zote nne za kwanza mfululizo, wakati Polisi ilipata pointi yao ya tatu kutokana na sare tatu huku ikiendelea kubaki mkiani mwa ligi ikiwa haina ushindi baada ya mechi 11. Imefungwa mechi 8.


Sare nyingine katika mechi za ugenini, ilionekana kumchanganya kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic ambaye alidai kwamba refa Jacob Ondongo kutoka Mara alichezesha vibaya na kwamba alionekana kuipendelea timu mwenyeji.


Kocha msaidizi wa Polisi, Ally Jangalu aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri akisema walikuwa na makosa katika upande wa ufungaji lakini wamerekebisha kiwango tangu walipocheza dhidi ya Ruvu Shootings ambapo walilala 2-1 kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.


Mgambo ambao waliwashikilia Simba katika sare ya kustusha mkoani Tanga iliyochangia kusimamishwa kwa kiungo wa Wekundu, Haruna Moshi 'Boban', walijikuta wakimaliza wakiwa 10 uwanjani baada ya beki wao Salum Mlima kumchezea rafu beki wa Yanga, Mbuyu Twite katika dakika ya 85 na kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro.


Coastal Union ya Tanga iliyo katika nafasi ya tatu itajaribu kuitetea nafasi yake wakati itakapocheza ugenini dhidi ya Azam iliyo katika nafasi ya nne kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi kesho.



Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa:

Yanga: 
Ally Mustapha 'Barthez', Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Athumani Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo/ Nurdin Bakari (dk.76), Didier Kavumbagu/ Jerry Tegete (dk.68), Hamisi Kiiza na Haruna Niyonzima.

Mgambo JKT:
Godson Mmasa, Salum Mlima, Yasin Awadh, Salum Kipanga, Bakari Mtama, Ramadhan Malima, Chande Maguja, Issa Kanduli/ Nassor Gumbo (dk.59), Fully Maganga na Juma Mwinyimvua/ Omary Matwiko (dk.76).


Vikosi kwenye Uwanja wa Jamhuri vilikuwa:
 
Polisi Morogoro:
Aghaton Mkwando, Nahoda Bakari, John Bosco/ Mokili Lambo (dk.28), Noel Msakwa, Hamis Mamiwa, Abdallah Mfuko, Bantu Admin, Maige Pascal, Ally Shomary, Malimi Busungu, Nicholaus Kabipe.

Simba:
Juma Kaseja,  Nassor Masoud 'Chollo', Amir Maftah, Pascal Ochieng, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa.        

No comments:

Post a Comment