Monday, October 1, 2012

WAREMBO REDD'S MISS TANZANIA 2012 KUINGIA KAMBINI KESHO

Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga (katikati) akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu shindano la Redds Miss Tanzania 2012. Warembo wa shindano hilo wataingia kambini kesho. Wengine pichani ni Meneja wa Bia ya Redds, Victoria Kimaro (kushoto) na Miss Tanzania 2011, Salha Israel (kulia).

WAREMBO 30 kutoka sehemu mbalimbali nchini wanatarajiwa kuingia kambini kesho kwenye hoteli ya Giraffe kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kushiriki shindano la urembo la Taifa 'Redd's Miss Tanzania 2012' litakalofanyika Novemba 3 kwenye ukumbi wa hoteli ya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency International, Hashim Lundenga alisema kuwa warembo wote walishapewa taarifa za kuripoti kambini kesho na mara baada ya kuwasili watapewa taratibu za kambi hiyo.

Lundenga aliwataka washiriki hao kuhakikisha wanawasili asubuhi mapema katika ofisi za Kamati ya Miss Tanzania kama walivyoambiwa ili wapelekwe pamoja katika hoteli hiyo iliyoandaliwa kwa ajili ya kambi yao ya mwezi mzima.

Alisema warembo wakiwa katika kambi ya Redd's Miss Tanzania watafundishwa mambo mengine muhimu katika maisha yao ambayo yatawafanya wajiandae kuwa wanawake walio na maendeleo na watakaokuwa tayari kuongoza familia zao.

Alisema pia baada ya kumpata mshindi atakapewa mapumziko ya miezi miwili na baadaye ataanza maandalizi ya kujiandaa kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia ya mwakani.

Alisema kuwa licha ya kuwapo na changamoto mbalimbali katika mashindano hayo, anawapongeza mawakala kwa kazi ya kusaka warembo ambao wengi wao waliofanikiwa kufuzu fainali hizo ni wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu.

No comments:

Post a Comment