Monday, October 8, 2012

VAN PERSIE AFUNGIWE KWA KUMPIGA 'KIPEPSI' CABAYE, ADAI KOCHA WA NEWCASTLE ALAN PARDEW

Refa Howard Webb (katikati) akiwaamua Robin van Persie (kushoto) wa Man U na Yohan Cabaye baada ya RVP kutuhumiwa kumchapa kiwiko kiungo huyo wa Newcastle.

KOCHA wa Newcastle United, Alan Pardew amesema chama cha soka cha England (FA) kinapaswa kuchukua hatua dhidi ya straika wa Manchester United, Robin van Persie.


Van Persie alihusika katika tukio la mbali na mpira dhidi ya kiungo wa Newcastle, Yohan Cabaye katika mechi ambayo Man U walishinda 3-0.


"Alimuangalia Yohan na akampiga kiwiko," alisema Pardew. "Nadhani jambo hilo linapaswa kuchunguzwa, kama nahitaji kuwa muwazi.


"Yohan asingeenda chini kama hakufanyiwa jambo lolote."


FA inaweza kulichunguza suala hilo kama refa Howard Webb hakuliona.


Pardew alisema hakuliona tukio hilo la kipindi cha pili baina ya mchezaji wa kimataifa wa Uholanzi, Van Persie na kiungo Mfaransa Cabaye wakati likitokea lakini aliona katika marudio ya video.


"Kuna historia kidogo ya kutokea mwaka jana na sijui kama Robin ameingia katika hilo, lakini kulikuwa  na chuki kidogo," aliongeza kocha huyo.


Manchester United walipanda hadi nafasi ya pili katika msimamo kutoka na ushindi huo.


"Ilikuwa ni mechi tuliyocheza vizuri," alisema kocha wa Man U, Sir Alex Ferguson, ambaye timu yake ililala 3-2 kwa Tottenham katika mechi yao iliyopita na ililala 3-0 dhidi ya Newcastle msimu uliopita.


"Tulidhamiria na umakini ulikuwa bab'kubwa. Si rahisi kuja Newcastle. Wao ni wakubwa, timu yenye nguvu na njaa ya ushindi."


Wageni waliokuwa mbele kwa magoli 2-0 ndani ya dakika 15 za kwanza shukrani kwa magoli ya vichwa kutoka kwa mabeki Jonny Evans na Patrice Evra.


Tom Cleverley kisha akaongeza la tatu kutokea mbali katika dakika ya 71, ingawa Ferguson anaamini kiungo huyo alikuwa akijaribu kupiga krosi.


"Sidhani kama Cleverley alijaribu kupiga shuti, lakini unayapokea mambo haya," alisema Mscotland huyo.
Ferguson pia aliwasifu mabeki wa kati Evans na Rio Ferdinand.


"Newcastle wanakulazimisha kucheza kwa kujituma," alisema. "Tulimudu tishio lao la mipira ya juu vyema. Rio Ferdinand na Jonny Evans walicheza vizuri sana."


Pardew anaamini kwamba magoli ya mapema ndiyo "yaliyoiua" timu yake.


"Hatukuweza kuyahimili," alisema. "Magoli yale mawili yalituua. Hata hivyo, katika dakika chache za kwanza za kipindi cha pili tulicheza vyema."

No comments:

Post a Comment