Tuesday, October 23, 2012

USAFIRI WA TRENI JIJINI DAR WAIVA... SASA ITAANZA SAFARI ZAKE KESHOKUTWA ALHAMISI IKIWA NA MABEHEWA SITA YATAKAYOBEBA ABIRIA 1,000... VITUO VITAKUWA KAMATA - BUGURUNI KWA MNYAMANI - TABATA MATUMBI - TABATA RELINI - MABIBO HADI UBUNGO MAZIWA... NAULI BADO!

Haya ... twende sasa...! Mfanyakazi wa Shirika la Reli (TRL), Elvis Mghase akiongoza jana treni itakayotumika kwa usafiri wa abiria kama daladala jijini Dar es Salaam kati ya Ubungo Maziwa na Kamata.  
Hatimaye usafiri wa treni itakayotumika kama daladala jijini Dar es Salaam utaanza rasmi kabla ya mwisho wa mwezi huu na huenda ikawa keshokutwa Alhamisi, imefahamika.
 

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kukagua miundombinu itakayotumika kwenye usafiri huo, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipalo Kisamfu, alisema kuwa ziara hiyo ililenga kukagua vituo, ukarabati wa mabehewa na pia pamoja na matuta ili kuepuka ajali

Kisamfu alisema kuwa treni hiyo itakuwa na mabehewa sita ambayo yenye uwezo wa kuchukua watu 1,000. Alivitaja vituo ambavyo treni hiyo itakuwa inasimama kuwa ni Kamata, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata Matumbi, Tabata Relini, Mabibo na Ubungo Maziwa.
 

Alisema kuwa tiketi za treni hiyo zitatengenezwa na kampuni ya Cellcom Wireless na zitakuwa zikiuzwa kwenye vituo ambavyo treni hiyo itakuwa ikisimama.

Kisamfu alisema kuwa kuna miundombinu bado haijakamilika lakini pamoja na hayo, usafiri huo utaanza kama ilivyopangwa huku ukarabati wa miundombinu mingine ukiendelea.

Hata hivyo, nauli za usafiri wa treni hiyo kutoka kituo kimoja hadi kingine bado haijatangazwa.


Chanzo: NIPASHE

No comments:

Post a Comment