Tuesday, October 23, 2012

HATUTAONA TENA MCHEZAJI KAMA MESSI KATIKA MAISHA YETU - VILANOVA

Leo Messi akishangilia goli alilofunga dhidi ya Real Madrid

KOCHA wa Barcelona, Tito Vilanova, kwa mara nyingine amemfagilia Lionel Messi – mfungaji wa 'hat-trick' kwenye Uwanja wa Riazor baada ya wikiendi ya mechi za kimataifa - kutokana na kiwango ambacho "hakuna mchezaji mwingine" anaweza kukionyesha.

Huku mbio za kuwania tuzo ya Ballon d'Or ya mwanasoka bora wa dunia zikiwa zimepamba moto, kocha huyo ana hakika kwamba Messi ndiye mwenye nafasi kubwa zaidi ya kutwaa tuzo hiyo, "sio kwa kile alichofanya juzi", akimaanixsha mechi dhidi ya Deportivo, "bali kwa sababu maisha yake yote ya soka". "Watu wanaopiga kura watapiga kura. Sitaki kupiga kampeni. Mmeona yakisemwa kila siku. Siku ile alionyesha kipaji chake. Hajawahi kutokea mchezaji aliyefunga 'hat-trick' kwenye Uwanja wa Riazor," alisema Vilanova katika mkutano na waandishi wa habari.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina amebakisha magoli manne tu kuifikia rekodi ya wakati wote ya kufunga magoli mengi zaidi katika mwaka mmoja (Januari-Desemba) inayoshikiliwa na Pele tangu mwaka 1959.

Alipoulizwa ni lini Messi ataipiku rekodi hiyo, kocha huyo wa Barcelona hakutaka kuzungumzia lakini alisifu kipaji cha mwanafunzi wake.

"Sijui nini kingine kitasemwa kuhusu Leo. Hatutakuja kumuona mchezaji kama yeye tena. Alithibitisha hilo siku ile, kucheza mechi ya ugenini na kucheza wakiwa 10 uwanjani (baada ya Mascherano kutolewa kwa kadi nyekundu). Alifanya juhudi ya mfululizo katika kushambulia na kulinda lango. Hebu tu-injoi vitu vyake kwa kadri tuwezavyo," alisema Vilanova.

No comments:

Post a Comment