Monday, October 8, 2012

TFF YAPONGEZA UONGOZI MPYA ARFA

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Oktoba 7 mwaka huu).

TFF kupitia kwa afisa habari wake, Boniface Wambura ilisema ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ARFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Kigoma.

Wambura alisema TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya ARFA chini ya uenyekiti wa Khalifa Mgonja ambaye amechaguliwa tena kuongoza chama hicho.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Arusha kwa kuzingatia katiba ya ARFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

"Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya ARFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF," alisema Wambura.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Khalifa Mgonja (Mwenyekiti), Seif Banka (Makamu Mwenyekiti), Adam Brown (Katibu), Peter Temu (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Omari Walii (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Mwalizo Nassoro (Mhazini).

Waliochaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi huo uliofanyika Leganga, Usa River ni Hamisi Issa, Athuman Mhando na Eliwanga Mjema. Nafasi ya Katibu Msaidizi iko wazi na itajazwa katika uchaguzi mdogo utakayofanyika baadaye.

No comments:

Post a Comment