Monday, October 8, 2012

MECHI YA SIMBA, OLJORO YAINGIZA MIL 46/-

Kipa wa JKT Oljoro, Shaibu Issa akidaka mpira mbele ya washambuliaji wa Simba wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Simba ilishinda 4-1.

Beki wa Simba, Nasoro Said Masoud 'Cholo' akiwania mpira dhidi ya Salim Mbonde wa JKT Oljoro wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Simba ilishinda 4-1.
Kipa wa JKT Oljoro, Shaibu Issa akidaka mpira wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Simba ilishinda 4-1.

Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto akiwa "sakafuni" wakati akiwania mpira dhidi ya Markus Raphael wa JKT Oljoro wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Simba ilishinda 4-1.

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Oljoro JKT ya Arusha iliyochezwa jana (Oktoba 7 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 imeingiza Sh. milioni 46.68.
 

Katika mechi hiyo, Simba ilipata magoli yake kupitia kwa Amri Kiemba aliyefunga magoli mawili, Emmanuel Okwi aliyekuwa akicheza kwa mara ya kwanxza baada ya kutumikia adhabu ya kadi na Felix Sunzu aliyefunga kwa penalti iliyotokana na kipa wa Oljoro, Shaibu Issa, kumdaka miguu Okwi aliyempiga chenga na kutaka kwenda kufunga. Oljoro walimaliza wakiwa tisa uwanjani baada ya wachezaji wao wawili kutolewa kwa kadi nyekundu, akiwamo kipa Shaibu.  

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF kupitia afisa habari wake Boniface Wambura, watazamaji 8,081 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.


Wambura alisema kila klabu ikipata mgawo wa Sh. milioni 8.2 (Sh. 8,172,396.61) wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 7,120,677.97.

Alisema mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 193,000, waamuzi sh. 210,000, mwamuzi wa akiba (reserve referee) sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.

Aliongeza kuwa gharama za umeme zilikuwa Sh. 300,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 3,500,000 wakati tiketi ni sh. 3,175,000. Gharama za mchezo sh. 2,724,132.20, uwanja sh. 2,724,132.20, Kamati ya Ligi sh. 2,724,132.20, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,634,479.32 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,089,652.88

No comments:

Post a Comment