Saturday, October 13, 2012

SIMBA YADONDOSHA POINTI TANGA, AZAM YAWASHA TAA NYEKUNDU

Picha iliyochukuliwa kutoka katika 'skrini' ya kituo cha StarTV ikiwaonyesha wachezaji wa Simba wakitoka vichwa chini wakati wa mapumziko ya mechi yao dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani jioni ya leo.

AZAM FC imepiga hatua kubwa kuelekea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom kufuatia ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Polisi mkoani Morogoro huku Simba ikidondosha pointi mbili katika sare ya 0-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mechi ambayo wenyeji walimaliza wakiwa 10.

Goli pekee kutoka kwa straika raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche liliifanya Azam ifikishe pointi 16, moja nyuma ya mabingwa Simba wenye pointi 17 huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa wamecheza mechi moja zaidi ya Azam.

Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Coastal Union walilazimika kucheza dakika 25 za mwisho wakiwa 10 baada ya straika wao nyota Nsa Job kutolewa kwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 65. 


Katika mechi nyingine za leo, kwenye Uwanja wa Manungu, wenyeji Mtibwa Sugar walichapwa 2-1 na timu ya Mgambo JKT ya Tanga, ikiwa ni ushindi wake wa pili mfululizo baada ya kuanza na vipigo vinne mfululizo tangu ilipopanda daraja msimu huu.

Ruvu Shooting ilishinda 1-0 dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi na Prisons ililala nyumbani 1-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
 
 Vikosi katika mechi ya Tanga vilikuwa:

Coastal:
Jackson Chove, Said Swedi, Juma Jabu, Mbwana Hamisi, Jamal Machelanga/Ismail Khamis, Jerry Santo, Mohamed Athumani/Daniel Lyanga, Selemani K Selemani, Atupele Green, Nsa Job na Razack Khalfan/Lameck Mbonde.    


Simba:
Juma Kaseja, Nassor Said 'Cholo', Pascal Ochieng, Shomary Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi ‘Boban’, Felix Sunzu, Daniel Akuffor/Salim Kinje na Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman.

No comments:

Post a Comment